Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa mwongozo Kusini Mashariki mwa Asia kujikwamua baada ya COVID-19

Mama na binti yake mwenye umri wa miaka miwili nyumbani kwao huko Java ya kati, Indonesia.
© UNICEF/Fauzan Ijazah
Mama na binti yake mwenye umri wa miaka miwili nyumbani kwao huko Java ya kati, Indonesia.

UN yatoa mwongozo Kusini Mashariki mwa Asia kujikwamua baada ya COVID-19

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kukabiliana na pengo la usawa, kuhakikisha usawa wa huduma ya kidijitali kwa wote, kuimarisha uchumi wa kijani, kudumisha haki za binadamu na utawala bora vitakuwa muhimu sana kwa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia katika kujikwamu vyema kutoka kwenye janga la virusi vya corona au COVID-19.

Katika taarifa yake ya kisera aliyoitoa leo ambayo inatathimini athari za janga la COVID-19 kwa nchi 11 za ukanda huo na mapendekezo ya jinsi ya kujikwamua  ambayo yanaweka usawa wa kijinsi kama kitovu cha hatua hizo Antonio Guterres amesema “Kama ilivyo katika sehemu zingine duniani afya, uchumi na athari za kisiasa za COVID-19 zimekuwa kubwa Kusini Mashariki mwa Asia na kuwaathiri vibaya zaidi wasiojiweza na walio hatarini.” 

Malengo ya SDG’s yanayumba 

Ukanda wa Kusini Mashariki mwa Asia zinajumuisha Brunei, Cambodia, Laos, Indonesia, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand, Timor Mashariki na Viet Nam. 

Katibu Mkuu amesema hata kabla ya janga la COVID-19 nchi hizo zilikuwa zinasuasua katika utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs ambayo ukomo wake ni mwaka 2030. 

Licha ukuaji imara wa uchumi taarifa hiyo ya kisera ya Guterres imeonyesha kwamba ukanda huo unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo pengo kubwa la usawa, kiwango cha chini kabisa cha hifadhi ya jamii, sekta kubwa isiyorasmi, na changmoto za kutokuwepo amani, haki na taasisi dhoofu.  

Zaidi yah apo mfumo mzima wa Maisha umeathirika, bayoanuwai inaendelea kupotea, na viwango vya utoaji hewa ukaa ya viwandani, na ubora wa hewa vitatoa hofu kubwa. 

Pengo la usawa na ongezeko la mivutano 

Bwana Guterres ameongeza kuwa “Janga la COVID-19 limedhihirisha pengo kubwa la usawa lililopo, mapungufu katika utawala na athari zake kwenye maendeleo endelevu. Pia limeonyesha bayana changmoto mpya ikiwemo amani na usalama.”  

Amesema hali ya sasa katika ukanda huo inaelekea kwenye mdororo wa kiuchumi na mivutano ya kijamii huku migogoro ya muda mrefu haijapatiwa ufumbuzi kutokana na kukwama kwa michakato ya kisiasa. 

“Serikali zote katika ukanda huo zimeunga mkono wito wangu wa usitishaji uhasama duniani kote  na ninazitegemea nchi zote Kusini Mashariki mwa Asia kubadili ahadi zao kuwa vitendo vya maana vitakavyoleta mabadiliko katika nchi zao.” 

Ushirikiano wa kikanda ni mzuri

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO siku ya Jumatano , virusi vipya vya corona vinavyosababisha COVID-19 viliibuka kwa mara ya kwanza huko Wuhan China mwishoni mwa mwaka 2019 na Machi mwaka huu kutangazwa kuwa janga la kimataifa. 

Duniani kote kumeripotiwa wagonjwa milioni 16.5 na vifo takriban 657,000. Wakati ugonjwa huo uliwasili Kusini Mashariki mwa Asia mapema kuliko sehemu zingine za dunia mkuu wa Umoja wa Mataifa amezipongeza serikali za ukanda huo kwa kuchukua hatua mapema kupambana na janga hilo. 

Kwa wastan walichukua siku 17 kutangaza hali ya dharura au kufunga kila kitu baada ya kupatikana kwa wagonjwa 50 wa COVID-19 kwa mujibu wa taarifa ya kisera ya Guterres ambaye ameongeza kuwa “Hatua za kuudhibiti ugonjwa huo zimewanusuru Kusini Mashariki mwa Asia na kuwapunguzia athari kubwa kama zilizoshuhudiwa kwingineko. Na pia ushirikiano miongoni mwao ulikuwa mzururi na imara.” 

Wafanyakazi wa kiwanda  huko Cambodia
ILO/Marcel Crozet
Wafanyakazi wa kiwanda huko Cambodia

Maeneo manne muhimu ya kuyafanyia kazi 

Katibu Mkuu amesisitiza maeneo manne ambayo yatakuwa muhimu sana kwa Kusini Mashariki mwa Asia katika kuhakikisha wanajikwamua vyema kutoka kwa janga la COVID-19 na kuelekea katika ukanda endelevu, wenye mnepo na jumuishi kwa ajili ya mustakabali wao. 

Mosi amesema kupambana na pengo la usawa katika kipato, hudum za afya na hifadhi ya jamii. Na hayo yatahitaji hatua za muda mfupi na mabadiliko ya sera ya hatua za muda mrefu. 

Pili Bwana. Guterres amezishauri nchi za ukanda huo kuziba pengo la kidijitali ili kusiwe na mtu yeyote atakayeachwa nyuma katika dunia hii iliyounganika sana kuliko wakati mwingine wowote. 

Tatu amesema kutokana na kutegemea sana makaa yam awe na viwanda vingine katika siku za nyuma anawachagiza kubadili uchumi wao na kuingia kwenye uchumi wa kijani ikiwemo kuzalisha ajira za siku za usoni. 

Na nne ameutaka ukanda huo kudumisha haki za binadamu, kulinda maeneo ya kiraia na kuchagiza uwazi mambo ambayo amesema yataleta tija katika kujikwamua vyema.

Kusongesha usawa wa kijinsia

Guterres amesisitiza kwamba juhudi zote hizi zinahitaji kusongesha usawa wa kijinsia , kushughuliki ukatili wa kijinsia na kuwalenga wanawake katika Nyanja zote za kujikomboa kiuchumi na mipango mingine. “Hili litasaidia kupunguza athari za janga la COVID-19 kwa wanawake na ni moja ya mambo muhimu katika maendeleo endelevu, lakini pia kujikwamua kwa haraka na ambako ni jumuishi kwa wote.” 

Ingawa changamoto hazikosekani Katibu Mkuu amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa umejizatiti kulisaidia eneo la Kusini Mashariki mwa Asia kufikia malengo ya SDGs na mustakabali wa amani kwa wote.