Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaongeza shida ya watoto wenye utapiamlo- UNICEF 

Watoto wa Cambodia wakipata mlo. Watoto kukosa lishe bora husababisha unyafuzi
World Bank/Masaru Goto
Watoto wa Cambodia wakipata mlo. Watoto kukosa lishe bora husababisha unyafuzi

COVID-19 yaongeza shida ya watoto wenye utapiamlo- UNICEF 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema kuwa nyongeza ya watoto milioni 6.7 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaweza kupata tatizo la kuwa na uzito mdogo zaidi kulingana na urefu wao na hivyo kuwa na unyafuzi kutokana na madhara ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19

Kwa mujibu wa uchambuzi uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Lancet, asilimia 80 ya watoto hao wanatoka nchi za Afrika zilizo kusini kwa jangwa la Sahara na Asia Kusini na kwamba zaidi ya nusu ni kutoka Asia Kusini. 

UNCEF inasema kuwa tatizo la uzito mdogo kulingana na urefu ni aina ya utapiamlo ambao unafanya watoto kuwa dhaifu na wanakuwa hatarini kufariki dunia na ukuaji wao unakuwa wa mashaka hata katika uwezo wa kujifunza. 

Shirika hilo limesema kuwa hata kabla ya COVID-19, watoto milioni 47 walikuwa tayari wana tatizo la uzito mdogo kulingana na urefu wao na idadi hiyo mwaka huu inaweza kufikia milioni 54, kiwango ambacho kitakuwa ni cha juu kuwahi kufikiwa. 

Uchambuzi huo unaonesha kuwa tatizo la uzito mdogo kulingana na urefu linaewza kuongezeka kwa asilimia 14.3 katika nchi za kipato cha chini na kati mwaka huu kutokana na madhara ya kiuchumi na kijamii ya COVID-19, na hivyo kuongeza vifo vya watoto wengine 10,000 kila mwezi hususani kusini mwa Afrika.  

Shirika hilo linaonya kuwa tatizo hilo ni chembe tu ya majanga yakumbayo watoto, likitana pia udumavu, utipwatipwa na utapiamlo miongoni mwa watoto, matatizo yatokanayo na lishe duni kutokana na huduma kuvurugwa wakati huu wa COVID-19. 

Mwanzoni mwa janga la COVID-19, UNICEF iliripoti kupungua kwa asilimia 30 kwa utekelezaji wa huduma zake za uokoaji wa maisha hususan zile za lishe ambapo katika baadhi ya nchi operesheni zimevurugwa kwa kati ya asilimia 75 hadi 100 kutokana na hatua za karantini za kuepusha maambukizi ya COVID-19. 

Mathalani nchini Afghanistan na Haiti, hofu ya maambukizi na ukosefu wa vifaa kwa wahudumu wa afya kumesababisha kupungua kwa kati ya asilimia 40 hadi 73 ya huduma za kupatia watoto lishe ili kukabili udumavu. 

Nchini Kenya, kiwango kimepungua kwa asilimia 40 ambapo duniani kote, zaidi ya watoto milioni 250 wanashindwa kunufaika na mgao wa vitamin A kutokana na hatua za kukabili kuenea kwa COVID-19. 

UNICEF kupitia kampeni  yake ya Reimagine, inataka serikali na wadau wake kuendeleza hatua za kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa, kwa mfano watoto waendelee kupata chakula hata mgao upelekwe nyumbani iwapo shule zimefungwa.