WHO yasaidia kurejesha kwa madaktari wa Azerbaijan ili wasaidie mapambano dhidi ya COVID-19 nchini mwao 

29 Julai 2020

Ikiwa ni sehemu ya msaada wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO kwa harakati za Azerbaijan kupambana na virusi vya corona au COVID-19, mradi wa REACT-C19 umewaleta madaktari 19 raia wa Azerbaijan waliokuwa wanafanya kazi Uturuki ili warudi nyumbani kusaidia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kuhusu jinsi ya kushughulikia COVID-19.

Mafunzo yamefanyika katika maeneo mengi ya nchi. Katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku, watalaamu wanafundisha namna zote za kupambana na virusi vya corona ikiwemo kusafisha mikono kwa kutumia vitakasa mikono.   

Mradi wa REACT-C19 ambao unalenga kuisaidia Azerbaijan katika kuongeza kasi ya uwezo wa utayari, umemaliza awamu yake ya pili na matokeo ya kufurahisha ukiwa umefikia hospitali 8 katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu. Mradi ulianza katikati mwa mwezi Aprili walipowasili madaktari 19 raia wa Azerbaijani ambao wanafanya kazi zao nchini Uturuki.  Dkt Hande Harmanci ni Mwakilishi wa WHO nchini Azerbaijan, “tulifikiria ni muhimu kwamba tunapaswa kuwaleta watu kusaidiana bega kwa bega na madaktari na waendeshaji wa hospitali ili tuweze kuziweka hospitali tayari na madaktari wakae sawa na kile wanachotakiwa kufanya katika kuwahudumia wagonjwa wa COVID-19.” 

Katika kipindi hiki cha mafunzo, zaidi ya wahudumu wa afya 400 wakiwemo madaktari, wauguzi na wafanyanyakazi wengine wa hospitali kama vile watu wa usafi, wapishi na wengineo, wamehudhuria mafunzo ambayo yametolewa na timu ya mradi wa REACT-19. 

Mbali na mafunzo na kuweka viwango vya huduma, timu pia imewasaidia madaktari wenyeji katika kushughulikia wagonjwa walioko katika hali tete ya kiafya. Dkt Sabir Israfilov ni mmoja wa wakufunzi, mshauri kutoka mradi huo wa REACT-C19, "kwa kweli kama walivyo raia wa Azerbaijani ambao wanaishi mbali na nyumbani, mara zote tunakuwa na mawazo kuhusu kuchangia kwa nchi yetu hata kama ni kidogo. Wote tuna hizi hisia ndani yetu. Katika kipindi cha virusi vya corona ambacho nchi yetu inapita katika nyakati ngumu, janga hili linalinganishwa na vita, kupewa nafasi katika kipindi hiki ni jambo kubwa kwetu. Na tumekuja hapa kupitia shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO.”  

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud