Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 5 wauawa na 9 kujeruhiwa katika shambulio Darfur:UNICEF

Wanawake na watoto waliotawanywa kutokana na mapigano  Jebel Marra,  Darfur Kaskazini, wakijihifadhi katika kituo kipya cha Tawilla
OCHA
Wanawake na watoto waliotawanywa kutokana na mapigano Jebel Marra, Darfur Kaskazini, wakijihifadhi katika kituo kipya cha Tawilla

Watoto 5 wauawa na 9 kujeruhiwa katika shambulio Darfur:UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limealaani vikali shambulio lililofanyika kwenye Kijiji cha Masterei Darfur Magharibi nchini Sudan na kukatili maisha ya watoto watano na kujeruhi wengine tisa.

Taarifa iliyotolewa leo na kaimu mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Mohammed Ould Bouasri imesema watoto wote waliokufa na kujeruhiwa ni wa umri wa kati ya mwaka mmoja na mitatu“Salamu zetu za rambirambi zinakwenda kwa familia na jamii nzima Kwa mujibu wa ripoti pia nyumba 1,500 zimechomwa moto na kuziacha familia nyingi bila malazi au huduma za msingi wakati huu Sudan ikiendelea kupambana na janga la corona au COVID-19” 

Ameongeza kuwa UNICEF inatoa wito kwa pande zote katika mzozo kuwalinda watoto wakati wote kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu. 

 Bwana Bouasria amesisitiza kwamba “Hakuna kinachohalalisha mashambulizi kwa watoto. UNICEF inatoa wito kwa serikali ya Sudan kuchunguza shambulio hili na kuwawajibisha wahusika kwa ukatili huo dhidi ya watoto.” Hivi sasa amesema watoto na familia katika eneo hilo wanahitaji msaada wa haraka wa matibabu na wa kisaikolojia. 

UNAMID yalaani vikali  

Nao mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID, ukilaani shambulio hilo umesema unatiwa hofu kubwa na ongezeko la karibuni la machafuko na mashambulizi dhidi ya wanaoandamana kwa amani, raia, jamii za vijijini na kwenye makambi ya wakimbizi wa ndani katika maeneo mbalimbali Kaskazini, Kusini na Magharibi mwa Darfur. 

UNAMID imesema inalaani vikali kupotea kwa maisha ya watu, kujeruhiwa na kutawanywa kunakosababishwa na mashambulizi hayo huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto. 

Imeitaka mamlaka ya Sudan kuwakamata wahusika na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria. Pia UNAMID imesema inasikitika kwamba matukio haya yanatokea wakati serikali ya Sudan na makundi yenye silaha wanang’ang’ana kufikia makubaliano ya amani katika jaribio la kuleta amani ya kudumu na utulivu kwenye jimbo la Darfur na Sudan nzima.

Mpango huo umesisitiza kwamba kujirudia kwa matukio kama hayo katika wakati huu kwenye historia ya Sudan kutachochea mgawanyiko zaidi na uhasama miongoni mwa jamii na kuathiri mafanikio yaliyopatikana katika kuleta mapinduzi.