Kenya imejitahidi kudhibiti nzige lakini tishio bado lipo Afrika Mashariki:FAO

28 Julai 2020

Kenya imepiga hatua kubwa katika kudhibiti nzige wa jangwani ambao walivamia eneo la Afrika Mashariki mapema na kwingineko mwezi February na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao ilioweka maisha ya mamilioni ya watu njiapanda hasa katika suala la uhakika wa chakula limesema shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.

Kwa mujibu wa taarifa ya FAO iliyotolewa leo mjini Roma Italia kati ya nchi 29 zilizokumbwa na nzige hao waharibufu 26 zimefanikiwa kuwadhibiti lakini tatu bado zinapambana zikiwemo Kenya , Somalia na Ethiopia. 

Hata hivyo shirika hilo linatumai kwamba katika siku chache zijazo zitasalia nchi mbili na ndani ya wiki tatu Kenya na Ethiopia nazo zitajikomboa kwa kiasi kikubwa. 

Pamoja na mafanikio hayo Cyril Ferrand kiongozi wa FAO wa masuala ya mnepo katika eneo la Afrika Mashariki ameonya kwamba nchi hizo zisibweteke kwani tishio la kuzuka upya mzunguko mwingine wa nzige wa jangwani mwishoni mwa mwaka huu bado lipo. 

Ameongeza kuwa miongoni mwa nchi zote 29 zilizokumbwa na nzige wa jangwani mwaka huu Kenya ndio iliyoathirika vibaya zaidi baada ya kutoshuhudia nzige kwa miaka 70 ikifuatiwa na Ethiopia, Somalia na Sudan Kusini. 

Nzige wa jangwani
WFP/Peter Louis
Nzige wa jangwani

Juhudi kubwa za FAO kwa kushirikiana na wizara husika za kilimo na chakula katika nchi zilizoathirika zimefanikisha kuokoa karibu ekari laki sita Afrika Mashariki na kuua nzige bilioni 400 hatua iliyozuia uharibifu mkubwa wa mazao. 

Bwana Ferrand amesema changamoto kubwa ya kukabili nzinge hao ni operesheni ya kupambana na kasi yao ya kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine  lakini pia nzige hao wamekuwa wakielekea katika maeneo ya vijijini sana na kusambaa kwa kasi mathalani Ethiopia ambako operesheni ya kuwadhibiti inahitaji njia zote za ardhini na angani. 

Na sasa janga la corona au COVID-19 limezidisha changamoto mfano kuwapa mafunzo maafisa wa kukabiliana na nzige nchini Kenya ambako kuna amri ya kutotembea kwa muda fulani imefanya idadi ya saa za  kufanya kazi ya kudhibiti nzige hao kupungua. 

Makadirio ya FAO ni kwamba kati ya Juni na Desemba mwaka huu kutakuwa na idadi kubwa ya watu wasio na uhakika wa chakula Afrika Mashariki kutokana na nzige wa jangwani pekee na ukiongeza na janga la COVID-19 hali itakuwa mbaya zaidi.  

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter