Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Pafu la Kijani” Ethiopia na harakati za kuhifadhi mbegu pori za kahawa.

Msitu wa hifadhi ya mazingira, Kafa nchini Ethiopia.
World Bank/Sue Pleming
Msitu wa hifadhi ya mazingira, Kafa nchini Ethiopia.

‘Pafu la Kijani” Ethiopia na harakati za kuhifadhi mbegu pori za kahawa.

Tabianchi na mazingira

Nchini Ethiopia watafiti wamechukua hatua kuhakikisha wanalinda mbegu pori ya kahawa aina ya Arabika ambayo iko hatarini kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
 

Benki ya Dunia inasema kuwa uhifadhi wa maelfu ya aina ya kahawa hiyo kwenye msitu mnene wa hifadhi wa Kafa, uliopo kilometa 460 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ni muhimu siyo tu kwa maelfu ya wapenda kinywaji cha kahawa duniani kote, bali pia kwa takribani watu milioni 15 nchini Ethiopia ambao vipato vyao vinategemea zao la buni.

Ethiopia ni ya tano duniani kwa uzalishaji wa kahawa na ya kwanza barani Afrika ikikadiriwa kuwa mwaka 2018 iliuza magunia milioni 7.5 ya kahawa yenye uzito wa kilo 60.

Katika msitu wa Kafa, miti ya mibuni ya kahawa aina ya Arabika inatumika kuzalisha aina mbalimbali za mibuna ambayo inastahimili magonjwa na mabadiliko ya tabianchi.

“Msitu huu ni shina la jeni ya kahawa,” anaeleza Mesfin Tekle mtaalamu wa maliasili na mratibu wa mradi wa uhifadhi wa bayonuai, unaosaidia kusimamia msitu wa hifadhi wa Kafa.

Anasema kuwa, “miche inayohimili magonjwa na mabadiliko ya tabianchi inapatikana katikati ya msitu mnene wa mibuni na hii inaweza kuendelelezwa na kisha kupandwa. Huu ndio umuhimu wa msitu wa mibuni,” anafafanua mtaalamu huyo huku akionesha maua meupe ya mibuni yaliyochanua na majani pacha.

Kahawa pori aina ya Arabika ikiwa inakaangwa nchini Ethiopia.
World Bank/Sue Pleming
Kahawa pori aina ya Arabika ikiwa inakaangwa nchini Ethiopia.

Msitu wa Kafa uliotangazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO mwaka 2010 kuwa eneo la kitaifa la mazingira, lina ukubwa wa ekari 760,000 na ni makazi ya watu milioni 1.

‘Pafu la Kijani’ la Ethiopia.

Eneo hilo pia linatambuliwa kama ‘pafu la kijani’  kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufyonza hewa ya ukaa inayochafua mazingira.

Bayonuai ya eneo hilo kando ya mibuni, miti mingine ya viungo kama vile hiliki na pilipili, kuna wanyamapori na ndege.

Punde baada ya eneo hilo kutangazwa la kitaifa la mazingira, Tekle anasema kuwa, “ukataji miti hovyo ulipungua haraka, na kwa kuwa mibuni haistahimili mabadiliko ya ghafla ya joto, kupungua kwa unyevunyevu kwenye udongo kungalihatarisha uhai wa mibuni.”

Sasa mradi wa Benki ya Dunia unasaidia jamii inayozunguka eneo hilo kupitia miradi mbadala  badala ya kukata miti kwa ajli ya kuuza mkaa au kwa ajili ya kupanua mashamba.

Tekle anasema kuwa mibuni nayo inaimarika kutokana na hali nzuri ya hew ana kwamba, “wanywaji wa kahawa, ile ladha wanayofurahia na harufu nzuri inatokana na mazingira asili. Iwapo mazingira inamozalishwa kahawa yanatunzwa, basi manufaa yake yatafika kwenye kikombe cha kahawa cha mnywaji, na watu watafurahia kahawa nzuri.”