Mapigano mapya Jonglei, Sudan Kusini yafurusha maelfu ya watu 

27 Julai 2020

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini, UNMISS umesema idadi ya familia zinazosaka hifadhi kwenye kituo chake huko Pibor jimboni Jonglei imeongezeka na kufikia 8,000 kufuatia mapigano mapya jimboni humo yaliyotokea tarehe 23 mwezi huu.
 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric akizungumza na wandishi wa habari kwa njia ya mtandao hii leo kutoka New York, Marekani, amesema kuwa, “kundi la watu wenye silaha walishambulia na kuteka kijiji cha Lekoangole, kilichopo kilometa 30 kutoka mji wa Pibor.”

Ameongeza kuwa kitendo hicho kilisababisha watu kukimbilia eneo lililo jirani na kituo cha Umoja wa Mataifa.

“Mazingira kwenye eneo hilo ni mabaya kutokanana mafuriko. Watu wamekimbilia pia maeneo mengine ambako hakuna malazi, chakula wala huduma za afya,” amesema Bwana Dujarric.

UNMISS imesema kuwa vikundi vyote vyenye silaha vimekuwa vikijihusisha na ghasia ambazo zimeongezeka tanu mwezi Desemba mwaka 2019.

Kwa kuzingatia hali hiyo amesema kuwa, “UNMISS imetoa wito kwa vikundi hivyo visitishe mapigano na vitenge maeneo salama kwa raia na kuruhusu kufanyika kwa maridhiano.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud