Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 baada ya azimio la UN, bado mabilioni ya watu wanakosa maji salama na huduma za kujisafi-Mtaalamu

Mtoto akinywa maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bakassi, Maiduguri, Nigeria  (13 Machi 2017)
UNICEF/Fati Abubakar
Mtoto akinywa maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bakassi, Maiduguri, Nigeria (13 Machi 2017)

Miaka 10 baada ya azimio la UN, bado mabilioni ya watu wanakosa maji salama na huduma za kujisafi-Mtaalamu

Afya

Miaka kumi baada ya Umoja wa Mataifa kutambua maji na kujisafi kuwa ni haki ya binadamu, mabilioni ya watu bado wanakosa maji salama ya kunywa na kujisafi, ameonya mtaalamu wa Umoja wa Mataifa hii leo mjini Geneva Uswisi.

Bwana Léo Heller ambaye ni mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa katika upande wa haki za binadamu za maji na kujisafi amesema, “janga la virusi vya corona limetufundisha kuwa kuwaacha nyuma watu ambao wako katika uhitaji mkubwa wa huduma za maji na kujisafi, kunaweza kusababisha janga la kibinadamu. Katika miaka 10 ijayo, haki za binadamu za kupata maji na huduma za kujisafi zinatakiwa kuwa kipaumbele ikiwa tunataka kujenga jamii za haki na utu.”  

Tamko la mtaalamu huyu linakuja siku moja kabla ya kutimia miaka kumi ya azimio namba 64/292 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililofikiwa tarehe 28 Julai 2010 ambapo nchi 193 ziliweka ahadi ya kuwahakikishia watu wote huduma za maji salama na kujisafi.  

“Nusu ya glasi ni tupu na nusu nyingine ni imejaa. Hatua iliyopigwa tangu mwaka 2010 inaweza kuonesha kasi ndogo  katika utekelezaji wa haki za binadamu za kupata maji na huduma za kujisafi lakini kwa hakika azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama hatua ya kuanzia, limechochea mikakati kadhaa na kuhimiza maendeleo kadhaa.” Amesema Léo Heller. 

Ingawa mengi yamefikiwa katika miaka 10 iliyopita, Heller aanasema, nchi haziko katika njia sahihi kufikia malengo ifikapo mwaka 2030. Mtu mmoja kati ya watatu kwenye sayari yetu bado anashindwa kupata maji salama ya kunywa na zaidi ya nusu ya idadi ya watu ulimwenguni wanashindwa kupata huduma salama ya kujisafi. Watu wengine bilioni tatu wanakosa vifaa vya msingi vya kunawa mikono na sabuni na maji, na zaidi ya watu milioni 673 bado wanajisaidia katika mazingira ya wazi, hali ambayo kila mwaka inasababisha vifo vya 432,000 kutokana na ugonjwa wa kuhara.