Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante sana UNICEF kwa kutuondelea adha ya maji:Wakaazi wa Paida DRC

Utoaji umeme wa jua hutoa maji kwa wakaazi zaidi ya 6,000 katika kambi ya wakimbizi huko Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria.
IOM/Sascha Pimentel
Utoaji umeme wa jua hutoa maji kwa wakaazi zaidi ya 6,000 katika kambi ya wakimbizi huko Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Asante sana UNICEF kwa kutuondelea adha ya maji:Wakaazi wa Paida DRC

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limewaondolea adha ya maji ya muda mrefu wakazi wa Paida jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambao walilazimika kutembea mwendo mrefu kusaka huduma hiyo muhimu kwa miaka mingi.

Katika eneo la Paida wakazi wamekuwa na shida ya kupata huduma ya amaji safi kwa miaka na mikaka ambayo si uhai tu bali inasaidia kupambana na maradhi ikiwemo sasa vita dhidi ya janga la corona au COVID-19.

Shukran zao zinakwenda kwa UNICEF ambayo imesikia kilio chao na sasa imeamua kuchimba kisima na kuwawekea pampu ya maji karibu na makazi yao. Na ili kuhakikisha usalama wa pampu hiyo na huduma endelevu imewawekea pia msimamizi kutoka katika jamii hiyo ambaye ni Jean-Pierre Nzanzu Mbusa

“Jamii hii ilikuwa na wakati mgumu sana kupata maji. Watu walilazimika kwenda bali kuyapata, lakini sasa tuna kisima hiki, kinatusaidia sana kwa sababu sasa tunapata maji hapahapa. Pia yanasaidia kituo chetu cha afya na sasa hakipati tena uhaba wa maji.”

Kwa mujibu wa UNICEF maji hayo safi na salama yameleta faraja kwa wakazi zaidi ya 2,500 wa eneo la Paida lakini pia yanasaidia hospitali, shule na hata wakazi wa maeneo jirani.

Miongoni mwa wanufaika wa huduma hii ni mama huyu ambaye anasema imerahisisha maisha yake na kumpa wasaa zaidi wa kukaa na watoto wake

“Jina langu ni Kayira Mbalimbali, nina umri wa miaka 28 na nina watoto watano.”

Kayira pamoja na wakazi wengine wa Paida mbali ya kuwapunguzia mwendo wa kusaka maji pia yamekuwa mkombozi hasa wakati huu wa COVID-19 kwani wanaweza kunawa mikono na maji tiririka na hivyo kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo lakini pia kuzuia kipindupindu.

Sasa timu ya UNICEF ina mpango wa kupanua wigo wa huduma hiyo na tayari imeanza kujenga tanki kubwa la maji ili kusaidia jamii nzima.