Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moto na kuyeyuka kwa barafu Arctic vyahitaji hatua za haraka dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:WMO 

Eneo lenye joto kali Siberia June 2020 ilikuwa juu zaidi ya kawaida
NASA Earth Observatory
Eneo lenye joto kali Siberia June 2020 ilikuwa juu zaidi ya kawaida

Moto na kuyeyuka kwa barafu Arctic vyahitaji hatua za haraka dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:WMO 

Tabianchi na mazingira

Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO leo limesema joto kali la kupindukia na la muda mrefu Siberia limesababisha sehemu ya Arctic kuwa na joto kuliko kawaida na kuchochea kuzuka kwa moto wa nyika kwa mwaka wa pili mfululizo huku likionya pia kuhusu kupungua kwa kasi kwa barafu baharini kwenye pwani ya Urusi. 

Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa kiwango cha joto Siberia kimekuwa zaidi ya nyuzi joto 5 katika kipimo cha Selsiyasi ,zaidi ya kiwango cha wastani tangu Januari hadi Juni na mwezi Juni kiliongezeka hadi nyuzi joto 10 katika kipimo cha Selsiyasi zaidi wa kile cha wastani. 

“Katika baadhi ya sehemu Siberia wiki hii kwa mara nyingine zimefikia kiwango cha juu cha nyuzi joto 30 katika kipimo cha Selsiyasi , hivyo imekuwa joto kali Siberia kuliko hata sehemu nyingi za Florida” amesema Clare Nullis msemaji wa WMO mjini Geneva Uswisi. 

Ameongeza kuwa “Tumekuwa na joto lisilo la kawaida na kwa miezi kadhaa sasa na hili limechochea moto mbaya Arctic na wakati huohuo tunashuhudia kupungua kwa barafu inayofunika pwani ya mwambao wa Arctic. Na makadirio ya jumla ya hewa ukaa inayotoka huko tangu Januari ni ya kiwango cha juu kabisa kushuhudiwa katika miaka 18 tangu ilipoanza huduma ya kufuatilia kiwango cha hewa chafuzi ya moto wa nyika.” 

Hali hiyo imefuatiwa kiwango cha joto cha kustua cha nyuzi joto 38 katika kipimo cha Selsiyasi  kwenye mji wa Urusi wa Verkhoyansk tarehe 20 Juni mwaka huu. Hii imethibitishwa na huduma ya shirikisho la Urusi ya ufuatiliaji wa utabiri wa hali ya hewa na mazingira (Roshyromet) na WMO iko katika mchakato wa kuanzisha kamati kutathimini uamuzi huo. 

Sababu ya ongezeko hilo la joto 

Sababu ya joto hilo kali la muda mrefu ni kuzuia hatua za masuala ya hali ya hewa kwenye ukanda wa Arctic Pamoja na kuvuma kwa upepo kuelekea upande wa kaskazini ambao umekuwa ukisukuma hewa ya moto kwenye ukanda huo. 

“Arctic inashika joto kwa kasi mara mbili ya viwango vya kimataifa vya wastani na kuathiri watu wa eneo hilo na mfumo mzima wa Maisha huku likiwa na athari kubwa” amesema Bi. Nullis na kuongeza kuwa ikiwango hicho kibaya cha joto kisingewezekana bila mkono wa shughuli za kibinadamu zinazochangia mabadiliko ya tabianchi. 

WMO imesema picha za video zinazoonyesha moto wa nyika unaokaribia kwenye bahari zimehimiza haja ya hatua za haraka za mabadiliko ya tabianchi zinazopaswa kuchukuliwa na mataifa na pia kuhakikisha ahadi zilizowekwa kwenye mkutano wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi zinafikiwa ikiwemo juhudi za kudhibiti kiwango cha ongezeko la joto duniani kusalia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi  juu ya ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya viwanda. 

Moto wa nyika katika picha za setilaiti zikionyesha sehemu za Siberia zinazoteketea
NASA Earth Observatory
Moto wa nyika katika picha za setilaiti zikionyesha sehemu za Siberia zinazoteketea

Athari za moto huo 

Takwimu zilizotolewa jana Jumatano na Roshydromet zinaonyesha kwamba kuna uwezekano wa maeneo 188 ya moto wa nyika Siberia, huku moto mkubwa zaidi ukishuhudiwa katika jamhuri ya Sakha na Chukotka iliyojitenga Kaskazini Mashariki mwa Siberia. 

Maeneo yote hayo yameshuhudia kiwango cha joto zaidi ya kawaida katika miezi iliyopita. Mamlaka ya Urusi pia imetangaza kwamba kuna hatari kubwa ya moto kwenye jimbo la Khanty-Mansiysk ambalo liko Magharibi mwa Siberia. 

WMO imeonya kwamba moshi wa moto wa nyika una uchafuzi mkubwa ikiwemo hewa ya cabrbon Monoxide, Nitrogen Oxide, baadi ya chembechembe ngumu na za aerosol. Na kwa mwezi juni pekee moto wa nyika wa Arctic umetoa megatani 56 za hewa ukaa ikilinganishwa na megatani 53 za Juni 2019. 

“Tunaona picha za setlaiti zikionyesha eneo lililoungua nab ado moto unaendelea kaskazini mwa arctic, na moto huo uko chini la kilometa nane kutoka kwenye bahari ya Arctic hili halipaswi kutokea.” Ameonya Bi. Nullis. 

Kutoweka kwa dubu wan cha ya kazikazini kunaendelea 

Msemaji huyo pia amekumbusha kwamba kupitia utafiti uliochapishwa kwenye jarida la masuala ya asili na mabadiliko ya tabianchi “dubu wa ncha ya kaskazini ambao wengi mnawafahamu kama nembo ya mabadiliko ya tabianchi wanaweza kuwa karibu kutoweka kabisa ifikapo mwisho wa karne hii endapo barafu baharini itaendelea kuyeyuka na kutoweka kwa kiwango cha sasa.