Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Picha moja nilimuuzia Rais George W Bush na nyingine Barack Obama kwa milioni 80-Masanja

Msanii wa kuchora kwa ktumia moto Washington Steven Masanja
UN/Washington Steven Masanja
Msanii wa kuchora kwa ktumia moto Washington Steven Masanja

Picha moja nilimuuzia Rais George W Bush na nyingine Barack Obama kwa milioni 80-Masanja

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai ilibaini kwamba ujasiriamali unaweza kuwa suluhu kubwa ya ajira kwa vijana na kusaidia jamii nyingi zisizojiweza hasa baada ya janga la corona au COVID-19 na ikatoa wito kwa serikali na wadau wengine kuondoa vikwazo kwa wajasiriamali.  

Nchini Tanzania, msanii wa uchoraji kijana Washington Steven Masanja anaishukuru serikali kwa kutambua kipaji chake na kumpa fursa ambazo zimemkwamua kiuchumi. Ingawa anajitambulisha tu kwa uchoraji wake wa kutumia moto ambao kimsingi unawasangaza wengi, kijana huyu ana vipaji vingine ukimwemo uchongaji katika miti na mbao ambavyo vyote vinampatia kipato kama anavyoeleza “awali nilikuwa nafanya kwa shilingi laki moja, na sasa hivi kazi yangu inaanzia shilingi milioni moja na kuendelea, ambayo ukiibadilisha unaweza kupata dola mia tano za kimarekani.” 

Je, soko lake ni lipi? Masanja anaeleza,  “soko langu linalenga kila jamii hususani watanzania kwasababu watu wengi wana mtazamo kwamba sanaa nyingi za ufundi wanauziwa wageni kutoka nje. Na mimi nasema ndivyo sivyo kwasababu kazi yangu haibagui na watanzania wanataka kile unachokifanya kiwe kina mamntiki katika jamii na kinafunza nini katika jamii.” 

Kazi za Washington Steven Masanja mara kwa mara zinatumika kuwapokea na kuwazawadia wageni wafikapo Tanzania kama anavyoeleza, “kwa mfano mwaka 2017 alikuja aliyekuwa rais wa Marekani George Bush akanunua kazi yangu kwa shilingi milioni 30 ambazo ni takribani dola elfu 12 za kimarekani, pia rais Barack Obama alikuja akanunua kazi yangu kwa shilingi milioni 50 ambayo inakaribia dola elfu 25 za kimarekani. Na ninajivunia kwamba watanzania wameweza kuzipokea kazi zangu kwa mfano ukiangalia pale katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa tatu ambao ni uwanja mpya ukienda katika eneo la kupokea mizigo kuna picha kubwa za wanyama watano wakubwa ‘Big Five’ na ninajivunia kuwa ni kazi za mikono  yangu. ” 

Pamoja na mafanikio hayo makubwa, kubwa zaidi analojivunia kijana huyu ni kuwahi kuiwakilisha nchi yake kimataifa, “mnamo mwaka 2019 nilichaguliwa kati ya watanzania wote nilikuwa mtu wa kwanza kwenda kuiwakilisha Tanzania nchini China ambako nilitembelea miji mbalimbali na kujifunza mengi kwa mwaka mmoja. Kuna mashindano yalifanyika barani Afrika, katika nchi 54 nikawa mshindi wa pili ambapo mshindi wa kwanza alikuwa anatoka Afrika kusini. Kwenye kipindi cham waka mmoja niliokuwa China nimejifunza mengi na ndiyo maana sanaa inasogea.” 

Mwisho, msanii Washington Steven Masanja ana ushauri kwa jamii? Naishauri jamii isiwe na fikira potofu kwamba sanaa za ufundi zinawalenga watalii. Hapana. Watalii wao wanakuja na kusema kile kitu ambacho wanakipenda na ndio maana wasanii wengi wanawatengenezea kwa ajili yao. Kwa hivyo wewe mtanzania ukija unataka kazi ambayo unaona wewe inakufaa, msanii anatengeneza.”