Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa inayosababishwa na vurugu Sudan Kusini inatishia maisha ya maelfu ya watu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP wamekuwa wakisambaza chakula katika mji wa Pibor, Sudan Kusini.
UNMISS/Tim McKulka
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP wamekuwa wakisambaza chakula katika mji wa Pibor, Sudan Kusini.

Njaa inayosababishwa na vurugu Sudan Kusini inatishia maisha ya maelfu ya watu

Amani na Usalama

Vurugu za mara kwa mara katika eneo la Jonglei na Pibor, mashariki mwa Sudan Kusini tayari zimewatawanya watu 60,000 na zinalemaza uhakika wa chakula na ustawi wa watu, mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la mpango wa chakula WFP na la chakula na kilimo FAO, yameonya kupitia taarifa iliyotolewa hii leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.

WFP na FAO zina wasiwasi kuwa vurugu hizo zimesimamisha ukulima, hali ambayo itaharibu mavuno kwa mwaka mzima.

“Pia vurugu hizo zimesababisha kuporwa kwa msaada wa chakula ambao ulikuwa unalenga kuwasaidia watu walioko hatarini.” Imesema taarifa hiyo.

Naye Mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini, Meshack Malo, amesema, “katika kilele cha msimu wa kupanda, kukosekana kwa usalama kunawazuia wakulima kwenda katika mashamba yao kuzalisha mazao ya chakula na wafugaji hawawezi kufuata njia yao ya asili ya kuhamahama ili kuilisha mifugo yao.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa WFP Sudan Kusini Bwana Matthew Hollingworth amesema, “hatuwezi kuwa na mbadala wa lishe ambayo maziwa yanawapatia watoto pale ambapo mifugo itakuwa imetoweka na tuna rasilimali chache kukabiliana na mahitaji ya sasa. Hakutakuwa na mshindi katika mgogoro huu: mgogoro huu unaweka hatari ya hali mbaya ya kukosekana kwa uhakika wa chakula kwa muda mrefu katika eneo hili kwa mwaka mzima.”

Aidha taarifa hiyo imethibitisha kuwa zaidi ya tani 430 za msaada wa chakula kutoka WFP imepotea kutokana na uporaji katika maghala ya WFP na wadau wake.