Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 19 kunusuru elimu kwa wakimbizi katika nchi 10 zikiwemo Kenya na Tanzania

Kakuma, kambi ya wakimbizi  nchini Kenya
UN/Esperanza Tabisha
Kakuma, kambi ya wakimbizi nchini Kenya

Dola milioni 19 kunusuru elimu kwa wakimbizi katika nchi 10 zikiwemo Kenya na Tanzania

Wahamiaji na Wakimbizi

Mfuko wa Elimu Haiwezi Kusubiri, ECW umetoa dola milioni 19 ikiwa ni awamu ya pili kwa ajili ya kushughulikia hatua za dharura za elimu kwa wakimbizi na wenyeji wao katika nchi 10 wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na mfuko huo imesema kuwa wanufaika wa fungu hilo ni wakimbizi na wakimbizi wa ndani katika mataifa hayo na hivyo kufanya jumla ya fedha zilizothibitishwa na mfuko huo kwa ajili ya kusaidia elimu katikati ya janga la corona kufikia dola milioni 43.5 huku nchi nufaika zikifikia 33.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu na mwenyekiti wa bodi ya ECW, Gordon Brown amesema kuwa, “wakati umefika kwa hatua thabiti za kuhakikisha kuwa kila mtoto mkimbizi anapata elimu bora. Mfuko wa Elimu Haiwezi Kusubiri unachukua hatua hizo na lazima tuongeze usaidizi wetu kwenye suala hili.”


Fedha hizo zitasambazwa na kutumia kwa ushirika baina ya serikali kuu, mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiraia katika nchi za Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Ethiopia, Iraq, Kenya, Lebanon, Libya, Sudan Kusini, Tanzania na Zambia.


Kwa ujumla wanufaika ni watoto na vijana wakimbizi wa ndani na wakimbizi wapatao 876,392 pamoja na jami wenyeji ambapo kati yao hao, 461,706 ni wasichana na 405,886 ni wavulana.

 

Kutokanana wakimbizi kushindwa kuendelea na masomo baada ya masomo kuvurugwa, msaada wa DCW unajumuisha watoto kuanzia wenye umri wa miaka 3 hadi 18 ambapo asilimia 23 ni wanafunzi wa elimu ya sekondari.


Ikichambua mgao wa fedha hizo, mathalani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itapatiwa dola milioni 2.3, Kenya Kenya dola milioni 2.3 kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na SAVE the Children.

 

Nchini Tanzania, dola milioni 1.5 zitaelekezwa kamati ya kimataifa ya uokozi, IRC ilhali Sudan Kusini dola milioni 2.3 zitakazotolewa zitaelekezwa shirikisho la kanisa la kiluteri duniani  na World Vision na Across.