Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa UN na haki za binadamu Tanzania  

Wasafiri kwenye basi la mwendo kasi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
UN-Habitat/Julius Mwelu
Wasafiri kwenye basi la mwendo kasi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Wataalamu wa UN na haki za binadamu Tanzania  

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wameisihi Tanzania iachane na hatua za kisheria na nyingine zinazobinya uhuru wa umma, hususan wakati huu ambapo taifa hilo la Afrika Mashariki linajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

Kupitia taarifa yao waliyoitoa leo mjini Geneva, Uswisi, wataalamu hao watatu, David Kaye, Clément Nyaletsossi Voule na Mary Lawlor wamesema ni kwa msingi huo wanaisihi serikali izingatie ahadi zake kuhusu haki za kibinadamu za kimataifa.
 
Wamegusia marekebisho ya hivi karibuni ya Sheria ya Usimamizi wa Haki za Msingi na Wajibu ambayo inataka yeyote anayesaka fidia kwa mujibu wao inarekebisha ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mujibu wa Sheria ya Haki za binadamu kuthibitisha kuwa binafsi ameathirika.
 
Marekebisho hayo, kwa mujibu wa wataalamu hao, yatazuia mashirika kufungua kesi kwa niaba ya waathirika, kwenye mazingira ambamo kwayo wamesema uwajibikaji na waathirika kupata haki ya kisheria ni tete.
 
“Marekebisho hayo ambayo yalipitishwa kwa haraka na Bunge bila mashauriano ya kina, ni miongoni mwa sheria zilizopitishwa hivi karibuni kutishia watetezi wa haki za binadamu, kunyamazisha uhuru wa vyombo vya habari na kudhibiti zaidi uhuru wa kujieleza, maandamano ya amani na kujiunga na vikundi kwa uhuru,” wamesema wataalamu hao.
 
Wito wa wataalamu hao huru umekuja baada ya kuchapishwa kwa malalamiko kuhusu sheria dhibiti na utekelezaji wa kina, yakiwemo malalamiko yaliyowasilishwa serikalini tarehe 24 mwezi uliopita wa Juni, kuhusu wasiwasi wa Utekelezaji wa sheria ya Haki za Msingi na Wajibu ambapo wataalamu wanahofia kuwa marekebisho hayo yatadhibiti uwezo wa mashirika ya kiraia na watu binafsi kutetea haki za makundi yaliyo hatarini, na jamii na hivyo kukiuka uhuru wa kujumuika.
 
Wataalam hao pia wamesema hatua hizo zinakuja huku pia viongozi wanane wa upinzani wakiwa wamekamatwa kwa kukusanyika kinyume cha sheria.
 
Wamesema vitisho na manyanyaso dhidi ya wanaharakati na wakosoaji wa serikali havikubaliki na hivyo viachwe mara moja.
 
TAGS: Tanzania, OHCHR