Mtoto DRC alima bustani kuimarisha lishe na mazingira

22 Julai 2020

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mtoto mwenye umri wa miaka 7 amechukua hatua ya kupanda bustani siyo tu kwa ajili ya kulinda mazingira bali pia kupata mlo pindi familia yake itakapokuwa haina fedha za kununua chakula.

Mtoto huyo Xavier Kaserka mkazi wa mji wa Goma, jimbo la Kivu Kaskazini anajivunia kuwa mmiliki wa bustani ambapo alipata fursa ya kumtembeza mgeni aliyevutiwa na bustani hiyo.

“Nimeotesha miti ya mipapai, miparachichi, miembe na miwa,” amesema Xavier huku akionesha miti hiyo ambayo tayari mingine ina matunda na migomba imeshabeba mikungu ya ndizi.

Xavier ambaye ni mwanamazingira, wakati wa ziara hiyo shambani amekutana na chupa ambayo amesema aliikota na kuanza kuzungumzia klabu ya mazingira ambayo yeye ni mwanachama.

UNICEF VIDEO
Mkungu huu wa ndizi kwenye bustani ya Xavier Karseka utavunwa siku si nyingi.

Anasema kuwa, “hii chupa itarejelezwa. Nitaipeleka kwenye klabu yangu ya mazingira na watatuelimisha jinsi ya kuzirejeleza na kisha tutaitumia tena na tena.”

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Xavier  mwenye shauku na bustani yake, akaenda mbali zai kufafanua kuhusu mipango ya mazao ya chakula kwenye bustani yake.

Xavier anasema kuwa, “ni kwamba pindi ndizi hizi zitakapokomaa tutazila. Nitakula maembe, nitakula maparachichi ambayo na nitakula pia malimau ambayo nitaotesha.”

Hivi sasa Xavier amekuwa mpaza sauti na mwakilishi kuhusu uendelezaji wa bustani binafsi katika ua akisema kuwa, “nawaeleza watu wapande vitu. Vitu unavyootesha vitakusaidia” Xavie akachuma jani la mboga na akiwa amelishika akasema, “hiki hapa ni chakula, hii inaweza kuwa mlo. Iwapo huna fedha, unaweza kupika na kula.”

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter