Vijana watatu nchini Tanzania wabuni mfumo wa kuweka umeme kwenye mita kwa njia ya simu

21 Julai 2020

Vijana watatu wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma nchini Tanzania waliobuni mfumo wa kununua na kuweka umeme kwenye mita kwa njia ya simu, wametoa wito kwa mamlaka za ndani ya nchi na kwingineko ulimwenguni kuwasikiliza na kuwapa nafasi za kuendeleza vipaji vyao.

Omary Muhaji ni mmoja wa vijana hao anaeleza kuhusu ubunifu wao mpya anasema, “Teknolojia hii ya sasa hivi inachofanya ni kuongeza thamani kidogo kwa mfumo wa sasa. Inaondoa usumbufu wa kuingiza zile namba kwenye mita za umeme. Kitakachotokea endapo umeme umekwisha au umepungua na mtu anahitaji kuongeza, anatumia njia ya kawaida kwa simu za kawaida na hatua ni zile zile kama mfumo wa sasa ulivyo, kwa hiyo ataingiza namba, ataingiza kiasi anachotaka kununua, akimaliza atathibitisha. Kwa hiyo mara baada ya kuthibitisha, umeme unaingia moja kwa moja.”

Baada ya hatua hii ya awali waliyoifikia, wana mpango gani? Omary Muhaji anaeleza, “ujuzi huu kwa sasa tuna mpango wa kuuendeleza, na kwa sasa hivi tuko chini ya Tume ya sayansi Tanzania, COSTECH, wao ndio wenye mamlaka ya kutusimamia na kutuingiza katika mfumo wa biashara kwa maana tuingie katika uzalishaji mkubwa zaidi na katika uhalisia”

Lakini wavumbuzi hawa wachanga wana neno kwa mamlaka na wadau wa sayansi na teknolojia duniani kote, kwa niaba ya wenzake, Muhaji anaeleza, "ningetamani kuona kwamba wanatusikiliza, vijana, manake naamini Tanzania kuna vijana wenye uwezo wa kufanya ambayo sisi tunafanya. Kwa hiyo mimi hoja yangu kuu ni kuwa watusikilize, kwa mfano uzalishaji wa mita za umeme ufanywe na watanzania tofauti na inavyofanywa sasa hivi kuagiza mita katika nchi za nje. Kingine ni kuunga mkono ubunifu mwingine ambao upo mtaani. Mimi ninaamini kuna ubunifu mwingi ambao vijana wanaufanya, wanachokikosa ni  jukwaa  ambalo linaweza kuwakuza na kuwaonesha katika vitu ambavyo wanavifanya. Kwa hivyo nadhani watu wenye mamlaka wawe wanakuja mtaani kuangalia vitu gani vinafanywa na vijana wa Kitanzania.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud