Jamii za watu wa asili ziko hatarini zaidi kwa COVID-19:WHO

20 Julai 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema ingawa watu wote wanaathirika na janga la corona au COVID-19 lakini watu mafukara na wasiojiweza wakiwemo jamii za watu wa asili wako hatarini zaidi na janga hili kote duniani bila kujali wako mijini au vijijini.

 

Katika mkutano wake kwa njia ya mtandao na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi, mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus amesema kuna watu wa asili takribani milioni 500 katika nchi zaidi ya 90 kama yalivyo makundi mengine yasiyojiweza wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Ameongeza kuwa ukiacha changamoto za kutokuwa na uwakilishi wa kisiasa, kutengwa kiuchumi, kukosa huduma za afya, elimu na za kijamii, watu wa asili mara nyingi pia wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa umasikini, ukosefu wa ajira, utapiamlo na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza hali ambayo inawaweka katika hatari kubwa zaidi ya janga la COVID-19 na athari zake.

Waathirika wakubwa.

Dkt. Tedros ameongeza kuwa ingawa COVID-19 ni hatari kwa watu wote wa asili duniani lakini WHO hofu yake kubwa ni athari za virusi hivyo kwa watu wa asili wa mataifa ya Amerika ambayo hivi sasa yanasalia kuwa kitovu cha janga hilo.“Hadi kufikia Julai 6 wagonjwa zaidi ya 70,000 wameripotiwa miongoni mwa jamii za watu wa asili katika nchi za amerika na vifo zaidi ya 2,000. Na hivi karibuni kabisa wagonjwa 6 wameripotiwa katika jamii ya watu wa asili wa Nahua wanaoishi katika eneo la Amazon upande wa Peru. Kwa sababu hiyo ofisi ya kanda ya Amerika ya WHO imechapisha mapendekezo kwa ajili ya kuzuia na kukabiliana na COVID-19 miongoni mwa watu wa asili na pia inashirikiana na waratibu wa mashirika ya watu wa asili ya bonde la mto Amazon ili kuweka mikakati ya mapambano dhidi ya COVID-19.

Mbinu za kudhibiti maambukizi

Mkuu huyo wa WHO amesema moja ya nyenzo muhimu za kudhibiti maambukizi miongoni mwa jamii za watu wa asili na jamii zote ni kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa. “Hakuna nchi ambayo itaweza kudhibiti mlipuko huo kama haitojua wapi virusi vilipo. Kama tulivyokwishasema mara nyingi hatua za watu kusalia majumbani zinaweza kusaidia kupunguza maambukizi lakini haziwezi kuukomesha kabisa ugonjwa huo. Kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa ni muhimu kwa kutafuta na kuwatenga walioambukizwa na kubaini na kuwaweka kwenye karantini watu waliokutana nao.”

Pia amesema apu mbalimbali za simu za mkononi zinaweza kusaidia kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa lakini hakuna kinachoweza kuwa mbadala wa kufuatilia watu mitaani, kwa wahudumu wenye mafunzo kupita mlango-kwa -mlango kutafuta waathirika na watu waliokutana nao na kukata mnyororo wa maambukizi.

WHO inasisitiza kwamba kufuatilia wagonjwa ni muhimu kwa kila nchi na kwa kila hali kwani kunaweza kusaidia kuzuia mgonjwa mmoja kugeuka kundi la wagonjwa na kundi hilo kuwa maambukizi ya kijamii. Na shirika hilo limesema hasa kwa wakati huu ambapo nchi nyingi zimeanza kurejea katika maisha ya kawaida hilo ni muhimu sana.

Muhimu kufuata mfano wa Ebola

WHO imesema kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupambana na milipuko ya magonjwa kuanzia ndui, polio hadi Ebola na sasa COVID-19.

Shirika hilo limesema moja ya mambo waliyojifunza kutokana na mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola ambao ulitangazwa kukomeshwa mwezi uliopita Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ni kwamba kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa kunawezekana hata katika mazingira magungu yenye changamoto za kiusalama.

Hivyo limesisitiza kuwa “Ebola na COVID-19 ni virusi tofauti lakini mingi ni ileile, haijalishi hali ni mbaya kiasi gani daima kuna matumaini. Kukiwa na uongozi imara, ushirikishwaji wa jamii na mikakati thabiti ya kudhibiti maambukizi na kuokoa maisha, COVID-19 inaweza kukomeshwa. Hatuhitaji kusubiri chanjo lazima tuokoe Maisha sasa. Na usifanye makosa , lazima tuendelee kuchapuza mchakato wa utafiri wa chanjo huku tukifanya kila tuwezalo kwa nyenzo tulizonazo.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter