Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yahitaji dola bilioni 10.3 kukabiliana na athari za kibinadamu za COVID-19

Familia eneo   la Kaya jimbo la Sanmatenge nchini Burkina Faso ikipata mlo baada ya kupokea mgao kutoka WFP.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Familia eneo la Kaya jimbo la Sanmatenge nchini Burkina Faso ikipata mlo baada ya kupokea mgao kutoka WFP.

UN yahitaji dola bilioni 10.3 kukabiliana na athari za kibinadamu za COVID-19

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na misaada ya kibinadamu leo yametoa ombi la dola bilioni 10.3 kwa ajili ya mikakati ya kimataifa ya kukabiliana na janga la corona au COVID-19 na athari zake.

 

Mwanzoni mwa mwaka huu taarifa hiyo imesema wahudumu wa misaada ya kibinadamu waliwalenga watu milioni 110 lakini leo hii wanahitakji kuwafikia watu milioni 250 na msaada wa kibinadamu katika nchi 63. 

Watu wengi zaidi wamejikuta katika hali mbaya na wanahitaji msaada wakiwemo watu masikini mijini, wanawake wasiojiweza na wasichana ambao wako hatarini kutokana na ukatili wa kijinsia, watu wenye ulemavu na matatizo ya afya ya akili, wazee, watu wenye njaa, watoto na vijana barubaru.

Umuhimu wa msaada wa fedha

Kwa mujibu wa OCHA mwezi Machi mwaka huu lilizinduliwa ombi la kimataifa kwa ajili ya hatua za kibinadamu za kupambana na COVID-19 ambapo dola bilioni 2 ziliombwa.

Lakini kutokana na ongezeko la mahitaji mwezi Mei ombi hilo liliongezeka na kufikia dola bilioni 6.7 na baada ya kuendelea kutathimini mahitaji na ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji msaada sasa ombi hilo limeongezeka na kufikia dola bilioni 10.3

Wakati wa mlipuko wa COVID-19 shirika la mpango wa chakula duniani WFP linagawa msaada wa kadi za fedha kwa familia 1,500 huko El Alto na La Paz, Bolivia
WFP/Morelia Eróstegui
Wakati wa mlipuko wa COVID-19 shirika la mpango wa chakula duniani WFP linagawa msaada wa kadi za fedha kwa familia 1,500 huko El Alto na La Paz, Bolivia

Mashirika hayo yamesema mipango ya ombi hili jipya ni ya kushughulikia  mahitaji ya msingi ya huduma za afya ikiwemo kujumuisha chanjo, huduma ya mama na mtoto  na mengineyo.

Lakini yamesema asilimia kubwa ya fedha hizo zitaelekezwa katika msaada ambao si wa afya hususani katika uhakika wa chakula, maji na usafi, kujikimu kimaisha, malazi na ulinzi ambao pia unajumuisha dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Ongezeko la watu wenye njaa

Kwa mujibu wa taarifa ya mashirika hayo hivi sasa linashuhudiwa ongezeko kubwa la watu wanaokabiliwa na njaa duniani ambao idadi yao inaweza kufikia milioni 270 ifikapo mwisho wa mwaka huu. Hivyo ombi hilo la leo linajumuisha dola milioni 500 za kuzuia baa la njaa.

Tangu kutolewa kwa ombi la kwanza la fedha OCHA inasema kufikia sasa ni dola bilioni 1.7 pekee zilizokwisha kusanywa ambazo hazitoshi hata kufikia mahitaji ya ombi la awali la dola bilioni 2 lililotolewa mwezi Machi.

Hata hivyo taarifa yao inatambua kwamba nchi zote zinaathirika kiuchumi na wahisani kwa ujumla wamejitolea zaidi katika kukabiliana na masuala ya kibinadamu kwenye nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2020 kuliko walivyofanya miaka ya nyuma ambapo mpaka sasa wameshatoa jumla ya dola bilioni 8.8 kwa ajili ya kukabiliana na masuala ya kibinadamu na COVID-19.

Taarifa yao imesisitiza kwamba kuichukulia hali kama mazoweya katika mazingira haya itakuwa ni hatari kubwa . Nchi tajiri zinalinda chumi zake na watu wake kwa misaada ya kuwapunguzia madhila lakini ni hatari kutowekeza katika kuwalinda walio hatarini zaidi duniani pia. Na isipofanyika hivyo basi taarifa imeonya kwamba kuna hatari ya kuwa na majanga mapya yaliyochochewa na COVID-19.

Wamesisitiza kwamba hakuna mtu katika dunia hii ambaye atakuwa salama dhidi ya virusi vya COVID-19 mpaka pale ambapo kila mtu atakuwa salama hivyo wametoa wito kwa dunia kuwa wakarimu sio tu kwa sababu ni jambo la kiutu kufanya lakini ni kwa sababu ni suala la maslahi yao.