Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziwa Albert lafurika, wakazi wahaha kujinusuru, COVID-19 yazidisha machungu

Yasmine Majid alikuwa anamiliki mgahawa ambao sasa umezingirwa na maji. Ametumia dola 1,600 kunusuru lakini haikusaidia chochote.
UN/ John Kibego
Yasmine Majid alikuwa anamiliki mgahawa ambao sasa umezingirwa na maji. Ametumia dola 1,600 kunusuru lakini haikusaidia chochote.

Ziwa Albert lafurika, wakazi wahaha kujinusuru, COVID-19 yazidisha machungu

Tabianchi na mazingira

Wakazi wa maeneo yanayozunguka Ziwa Albert nchini Uganda, wameomba serikali ichukue hatua kuwanusuru na janga la kufurika kwa maji ya ziwa ambalo sasa limesababisha nyumba zao kutwama kwenye maji, huku huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zikizamishwa kwenye maji.

Katika ufukwe wa Butiaba ulio mkubwa zaidi kwenye Ziwa Albert ambao ni makazi ya kituo cha polisi wanamaji wa ziwa hili na kile cha uhamiaji, kinachoshuhudiwa ni kiwango kikubwa cha maji, na watu waliokosa makazi, wakiwa hawana la kufanya, miundombinu ya umma vikiwemo vituo vya afya, hoteli na makazi vimeharibika.Hamna dalili kwamba mafuriko yatarudi nyuma kutokana na kukaribia kwa msimu wa mvua wa mwezi Septemba na Oktoba.

Jirani wa karibu Butyaba Green Beach Resort ni diwani mwanamke wa wilaya ya Buliisa, Robina Mulimba ambaye anasema kuwa, “biashara sasa hapa hakuna tena. Niliona maji yanajaa kwenye ufukwe na kwenye hoteli yake na mimi nikiwa kiongozi nikamweleza kuwa sasa atoke hapo ili hali isiwe mbayá zaidi. Alikuwa anasaidia sana eneo hili, biashara nyingi imeenda kwa maji. Mvua hakuna lakini tunaona maji yanajaa kila siku. Unahamia hapa na pale lakini hakuna msaada.”

Kwa kutambua kuwa hali si shwari na hata maeneo ya Kalolo, Bugoigo hali si shwari, diwani Mulimba anasema kuwa, “tumeshaandika barua nyingi kwa ofisi ya majanga, na wanatuma watu lakini bado hatujaona chochote. Hapa tulikuwa watu 1,500 lakini sasa imepungua. Hali ya hospitali ni mbayá kwa sababu maji yamefika , barabara imesombwa lakini sasa inabidi uchukue mtumbwi uende hospitali na watu hawana fedha. Wajawazito ni shida zaidi, huko, shida ni kubwa sana kuliko wanavyofikiria walio juu.”

Mtoto akiwa juu ya lundo la mchanga ambao hutumiwa na wakazi wa eneo hili kujaribu kuzuia maji ya ziwa Albert yasiingie kwenye makazi yao.
UN/ John Kibego
Mtoto akiwa juu ya lundo la mchanga ambao hutumiwa na wakazi wa eneo hili kujaribu kuzuia maji ya ziwa Albert yasiingie kwenye makazi yao.

Kuelekea Wanseko, takribani kilometa 150 kutoka hapa,  mfanyabiashara aitwaye Yasmine Majid amepoteza shilingi milioni 6 akijaribu kudhibiti mafuriko ya Ziwa Albert.Bi. Majid anasema kuwa, “tuliona kama maji yanakuja pole pole, tunachanganya udongo na kokoto na kuweka kwenye gunia na kufunga lakini mwisho wake tukaona inatushinda nguvu, kazi ya kula inatushinda. Miezi mitatu na nusu na tunahangaika kuzuia maji tukidhani kuwa yatatuacha.”

Huu si msimu wa mvua, hakuna mvua zinanyesha, lakini tunashangaa maji ya Ziwa Albert yanazidi kujaa na kufurika kila uchao - Robina Mulimba, Diwani  Buliisa

Bwana Dismas ni mmoja wa viongozi wa serikali ya mitaa, Wanseko yeye anasema kuwa tangu azaliwe haona shida kama hiyo na wito wake wakati huu ambao eneo lao linakumbwa na janga baada ya janga kuanzia nzige, kisha homa ya manjano, sasa Corona na sasa mafuriko ni kwamba “tunaomba serikali kama inaweza kufungua hii karantini ya COVID-19 hapa Buliisa kama wilaya nyingine. Hiyo ndio shida kubwa sana. Tunaomba wafungue pia Buliisa ili watu watembee, ile ya kuokoa watu ziwani imetwama, ofisi ya uhamiaji, soko letu kubwa pia la samaki nalo sasa liko majini. “

Kando na haya kivuko kilichokuwa kinasaidia kusafirisha bidhaa kutoka eneo la Bunyoro hadi mto Nile magharibi, nacho kimesitisha safari zake kutokana na bandari yake kufunikwa na mafuriko.

Shule zilizofungwa kwa sababu ya COVID-19 zimegeuzwa makazi kwa waliokosa malazi, na hawajui watakuwepo siku ngapi kwa kuwa maji yanawasogelea kila uchao.Naibu Waziri wa huduma za umma, David Karubanga, amesema wanatathmini athari za janga hili kabla ya kutoa msaada hivi karibuni. Bwana Karubanga akiongea kwa njia ya simu anasema kuwa, “shida iliyopo ni kwamba, wakati tulipata shida hiyo, tulikuwa tunakaribia mwisho wa mwaka wa fedha wa serikali. Kwa hiyo wakifungua hazina tutawanunulia vifaa, wasife moyo, rais alitoa amri wanunuliwe vifaa, lakini haiwezekani sasa hivi kwa sababu tulikuwa tunafunga mwaka wa fedha.”