Skip to main content

UNICEF na wadau wanusuru watoto na unyafuzi Madagascar

Sambazaffe kutoka Madagascar,  akiwa amembeba binti yake Sarah mwenye umri wa miezi 10 na ambaye ana unyafuzi.
UNICEF VIDEO
Sambazaffe kutoka Madagascar, akiwa amembeba binti yake Sarah mwenye umri wa miezi 10 na ambaye ana unyafuzi.

UNICEF na wadau wanusuru watoto na unyafuzi Madagascar

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na serikali ya Madagascar ili kunusuru watoto waliokumbwa na utapiamlo uliokithiri ambao umesababishwa na ukame wa muda mrefu kusini kwa taifa hilo.
 

Takwimu za UNICEF zinaonesha kwamba takribani watoto milioni 2.5  nchini Madagascar wenye umri wa chini ya miaka mitano, sawa na asilimia 6 ya watoto wote wana utapiamlo wa kupindukia au unyafuzi.

Sambezaffe ni mama wa watoto 10 ambapo mmoja wao ni Sarah Volafeno mwenye umri wa miezi 10 ambapo anasema kuwa, “watoto wangu wote 10 walipata unyafuzi. Kila mwaka hatuna chakula cha kutosha kulisha familia. Uhaba wa chakula ndio sehemu ya maisha yetu.”

Kutokana na hali hii, UNICEF kwa msaada wa fedha kutoka serikali ya Japan, inatekeleza miradi kadhaa ya kuimarisha lishe kwa familia.

Kusini Madagascar ambako kumekabiliwa na ukame wa mara kwa mara
FAO/Luc Genot
Kusini Madagascar ambako kumekabiliwa na ukame wa mara kwa mara

Sougrah Myriam Issa ni afisa wa kituo cha afya na anasema, “tunashirikiana na mawakala wa jamii ili kusimamia masuala ya lishe kwa wananchi. Tunafundisha wazazi jinsi ya kubaini watoto wao wenye unyafuzi, na wakibainika wanaelekezwa haraka kwenye kituo cha karibu cha afya au hospitali. Pia tunatumia kliniki za kwenye magari kufikia jamii zilizo maeneo ya ndani zaidi, mfano kilometa 10 kutoka kituo cha afya.”

Kwa kuwa uhaba wa maji pia ni sababu ya unyafuzi, UNICEF inahakikisha kuwa familia zinapata maji safi na salama kutoka vituo vya afya. 

Kutokana na mradi wa UNICEF sasa Sambezaffe anasema kuwa, “kupata huduma za afya, kunatupatia maisha bora kwa kuwa tunanufaika na mipango hiyo.”

Japan tangu mwaka 2016 imekuwa inatekeleza mpango wa chakula na lishe kwa nchi za Afrika, IFNA.