Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

COVID-19  yakosesha watoto huduma muhimu ya chanjo

© UNICEF/Thomas Nybo
Muuguzi akiandaa chanjo ya kuchanja mtoto katika kliniki Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

COVID-19  yakosesha watoto huduma muhimu ya chanjo

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na lile la kuhudumia watoto, UNICEF, hii leo wameonya juu ya ongezeko la idadi ya watoto wasiopatiwa chanjo za kuokoa maisha kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

 

Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo iliyotolewa leo katika miji ya Geneva, Uswisi na New York Marekani, imenukuu takwimu mpya za mashirika hayo zikionesha kuwa kuvurugwa kwa mipango ya chanjo kunatishia mafanikio yaliyopatikana kwa mbinde baada ya miongo kadhaa ya changamoto za kufikisha chanjo kwa watoto na barubaru.
“Mafaniko kama vile ya kupanua wigo wa utoaji wa chanjo dhidi ya saratani ya kizazi, HPV katika nchi 106 yanaweza kuporomoka,” yamesema mashirika hayo  yakiongeza kuwa, “mathalani katika miezi minne ya mwanzo yam waka 2020,  kumekuwepo na anguko la idadi ya watoto wanaokamilisha chanjo tangu muhimu za awali dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro au DTP3. Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 28 ambapo dunia inashuhudia kupungua kwa utoaji wa chanjo hii katika nchi zote.”

Muuguzi akiandaa shindano kwa wanakijiji wanaoleta watoto wao kupokea chanjo huko Vientiana Jamhuri ya Laos
UNICEF/Jim Holmes
Muuguzi akiandaa shindano kwa wanakijiji wanaoleta watoto wao kupokea chanjo huko Vientiana Jamhuri ya Laos

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa, “chanjo ni mbinu thabiti katika historia ya afya ya umma na watoto wengi zaidi hivi sasa wanapatiwa chanjo kuliko wakati wowote ule. Lakini janga la coronavirus">COVID-19 linaweka mafanikio hayo hatarini.  Machungu yanayoweza kuepukika sambamba na vifo vitokanavyo na watoto kukosa chanjo za kwenye mzunguko yanaweza kuwa makubwa zaidi kuliko coronavirus">COVID-19 yenyewe.”

Ameesma kuwa hali haipaswi kuwa hivyo na kwamba chanjo zinaweza kufikishwa kwa usalama hata wakati wa janga la Corona na hivyo anatoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa ratiba za mipango ya utoaji wa chanjo zinaendelea.

Mhudumu wa afya aktioa chanjo ya polio kwa mtoto Kaloko, Ndola, Zambia.
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Mhudumu wa afya aktioa chanjo ya polio kwa mtoto Kaloko, Ndola, Zambia.

COVID-19 imevuruga ratiba za chanjo

Kutokana na janga la Corona, takribani kampeni 30 za chanjo dhidi ya surua zilikuwa hatarini kusitishwa na hivyo kusababisha uwezekano wa milipuko ya surua kwa mwaka huu wa 2020 na zaidi. Utafiti wa UNICEF, WHO na fuko la chanjo duniani, GAVI, umeonesha kuwa asilimia 75 ya nchi 82 ziliripoti kuvurugwa kwa kampeni zao za chanjo hadi kufikia mweiz Mei mwaka huu.

Sababu zinatofautiana kuanzia watu kushindwa kufikia huduma za chanjo hata pale zinapokuwepo kwa hofu ya kuogopa kutoka nyumbani, ugumu wa maisha na karantini.

Hatuwezi kuzuia gonjwa moja na kuhatarisha harakati za kudhibiti lingine- Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji UNICEF

Wahudumu wa afya nao wengi wao hawakuwepo kwenye vituo vyao kutokana na vikwazo vya kutembea au kupelekwa katika maeneo mengine ya kushughulikia wagonjwa wa COVID-19.

“COVID-19 imesababisha ratiba za chanjo kukumbwa na changamoto kubwa,”  amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF akiongeza kuwa “ni lazima tuepushe kudorora zaidi kwa utoaji wa chanjo kabla maisha ya watoto hayajatishiwa zaidi na magonjwa mengine. Hatuwezi kuzuia gonjwa moja na kuhatarisha lingine.”

Je UNICEF na WHO wanafanya nini kunusuru?

Wakati huu ambapo jamii ya sekta ya afya dunian inahaha kutoa huduma katikati ya janga la COVID-19, UNICEF na WHO wanasaidia nchi katika juhudi zao za kujipanga vyema kwenye utoaji chanjo ambapo mashirika hayo, yanasaidia kurejesha huduma ili nchi hizo ziweze kurejesha ratiba za mzunguko wa chanjo kwa kuzingatia kanuni ya kutochangamana na kuwapatia wahudumu wa afya vifaa vya kujikinga.

Pili wanasaidia wahudumu wa afya kuwasiliana vyema na walezi kuelezea jinsi gani huduma zinazotolewa zinazingatia usalama. Tatu kufanyia marekebisho utoaji chanjo na pengo la kinga na kupanua wigo wa huduma na kufikia jamii ambazo ziko ndani zaidi na zilizo hatarini kukosa chanjo.