Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wachimba madini Venezuela walikatwa viungo na hata kuzikwa wakiwa hai- Ripoti

Sampuli ya dhahabu iliyochukuliwa kutoka mgodi.
© UNICEF/Claudia Berger
Sampuli ya dhahabu iliyochukuliwa kutoka mgodi.

Wachimba madini Venezuela walikatwa viungo na hata kuzikwa wakiwa hai- Ripoti

Haki za binadamu

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuhusu utumikishaji wa kupindukia na unyanyasaji wa watoto na jamii za watu wa asili kwenye machimbo ya madini ya dhahabu na madini mengine nchini Venezuela.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amejulisha nchi wanachama kupitia ripoti ya ofisi yake kwamba,  mamlaka za Venezuela zimeshindwa kuchunguza uhalifu kwenye sekta hiyo ya madini katika maeneo ya Arco Minero del Orinoco, ambako wachimba madini wanakatwa viungo na hata kuzikwa wakiwa hai.

Kupitia ripoti iliyoandaliwa na ofisi yake, Bi. Bachelet amesema licha ya uwepo kwa jeshi la Venezuela, yadaiwa kuwa makamanda wanalipwa hongo na yote hayo yanawezekana kufichika kwa sababu waajiriwa kwenye machimbo hayo ni wafanyakazi wasio na stadi za kutosha wanaolazimishwa kufanya kazi kwenye machimbo yasiyo salama kwa zamu ya saa 12.

Uhalifu huu lazima ukome

 “Mamlaka lazima zichukue hatua za haraka kukomesha ajira hizi zinazokiuka haki na ukatili wa kingono, ajira kwa watoto na usafirishaji wa binadamu na lazima zivunje magenge ya kihalifu yanayodhibiti shughuli za uchimbaji madini,’ amesema Bi. Bachelet kwenye taarifa yake.

Halikadhalika amesema ni lazima wachunguze, wafungulie mashtaka na wawaadhibu wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu mwingine.

Shuhuda zilizomo kwenye ripoti hiyo ya Umoja wa  Mataifa zinaonesha kuwa, wachimba madini ambao wanakiuka amri zilizowekwa na magenge hayo ya kihalifu walikuwa wanaadhibiwa vikali.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inatokana na ombi la jukwaa la Geneva kufuatia madai ya ukiukwaji wa haki wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Venezuela mwanzoni mwa mwaka 2014.

Yaelezwa pia kuwa wapingaji wa amri za magenge hayo ya kihalifu walikuwa wanapigwa risasi kwenye mikono au mikono yao ilikatwa sambamba na hata wengine kuuawa.

Maziko ya pamoja

 “Shuhuda mmoja ameelezea jinsi maiti walivyokuwa wanarusha kwenye mashimbo huku ghasia zikiripotiwa mara kwa mara baina ya magenge hayo wakati yakigombania umiliki wa machimbo,” imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne watu 149 wameuawa katika matukio kama hayo 16.

Ukahaba na usafirishaji wa binadamu

Utafiti na mahojiano yaliyofanywa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, vimedokeza kuwa wanawake pia walikuwa wanafanya kazi za uchimbaji na nyinginezo huku kukiwepo na ongezeko kubwa la ukahaba, ukatili wa kingono na usafirishaji wa binadamu wakiwemo barubaru.

Halikadhalika ,mazingira ya kuishi kwenye maeneo ya machimbo yalikuwa ni duni huku kukiwa na ukosefu wa maji, umeme na huduma za kujisafi.

Mahakama dhahifu

Ripoti pia imeelezea ukiukwaji wa haki hasa kwenye mauaji kinyume cha sheria na ukandamizaji wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro mwaka 2014.b

Imesema kuwa taarifa kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali inadokeza kuwa tangu mwezi Agosti 2017 hadi Novemba 2019, uchunguzi ulianza dhidi ya wanajeshi 766 ambao kati yao hao, 505 walishtakiwa, 306 waliswekwa ndani na 127 walifungwa.

Hata hivyo kuna kucheleweshwa kwa uendeshaji wa kesi kulikosababishwa na waendesha mashtaka na majaji wengi kuacha kazi sambamba na kuingiliwa kisiaasa kwa mahakama.