Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji sio wasambaza COVID-19 ni wapambana na COVID-19:IOM

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM Antonio Vitorino
Video Capture
Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM Antonio Vitorino

Wahamiaji sio wasambaza COVID-19 ni wapambana na COVID-19:IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema wahamiaji katika sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakinyanyapaliwa kama waeneza virusi vya janga la corona au COVID-19 suala ambalo ni kinyume na hali halisi.

Akizungumzia jambo hilo mjini Geneva Uswisi wiki hii mkurugenzi mkuu wa IOM Antonio Vitorino amesema wakati mamilioni ya watu wakisalia majumbani katika harakati za kupambana na COVID-19 wahamiaji wamekuwa kazini katika sekta mbalimbali muhimu kwa jamii hususan za afya na huduma za viwandani. Hivyo amesema sula hili“Ni moja ya masuala yanayoitia IOM wasiwasi, kwamba katika maeneo mbalimbali janga hili linatumika kuwanyanyapaa wahamiaji kama wasambaza virusi. Lakini ukweli ni kwamba wahamiaji na watu wenye asili ya uhamiaji wako msitari wa mbele katika vita dhidi ya ugonjwa huu, katika nchi kama Uingereza , Marekani na Canada takribani asilimia 30 hadi 40 wale walio msitari wa mbele katika huduma za afya ni wahamiaji au watu wenye asili ya uhamiaji.”

Ameongeza kuwa hata Uswisi na Italia bado sehemu kubwa ya wahudumu wa afya karibu asilimia 50 ni watu wenye asili ya uhamiaji au wahamiaji. Na ni muhimu kutambua kwamba katika nchi nyingi kila kitu kimefungwa lakini maisha yanaendelea katika sekta muhimu na huduma za msingi zinapatikana , hilo ni asante kwa wahamiaji kwani

“Hizo ndizo sekta ambazo wahamiaji wamebeba jukumu muhimu katika huduma za kufikisha bidhaa, huduma za usafirishaji, za masoko ya chakula na  nina uhakika kwamba nyote mmeshuhudia jukumu linalofanywa na wahamiaji katika kipindi ambacho wote tumesalia majumbani tukiogopa virusi lakini wao walikuwa hapo wakifanya kazi kwa faida ya jamii nzima.”

Kwa mantiki hiyo ameitaka jumuiya ya kimataifa kutambua kwamba mchango wa wahamiji ni mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na katika nchi nyingi kwani  bila wahamiaji zitataabika.