Kupambana na COVID-19 maji si uhai tu ni lazima:UNICEF

14 Julai 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema katika kupambana na janga la virusi vya corona au COVID-19 ni muhimu kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya maji ambayo si uhai tu bali ni lazima

Akizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa kisiasa (HPLF) unaofanyika kwa njia ya mtandao kuhusu malengo ya maendeleo endelevu SDG’s likiwemo lengo namba 6 la huduma ya maji safi na usafi (WASH), mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema janga la COVID-19 limedhihirisha pengo lililopo duniani katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu katika maisha ya binadamu na hasa kwa uhai wa watoto “Janga la COVID-19 limeanika wazi udhaifu wa huduma ya maji na usafi kote duniani, hususan kwa jamii masikini, kwa wasichana na kwa jamii na nchi zilizo katika migogoro. Huduma za WASH ni muhimu sana katika kuzuia maambukizi”

UN
Watoto watatu wakiosha mikono yao na maji kutoka kwenye bomba la maji, India. WHO / Tom Pietrasik

Katika mjadala huo wa ngazi ya juu ulioanza Jumatatu Bi.Fore ameongeza kuwa pamoja na kufahamu umuhimu wa huduma hiyo bado katika nchi 60 zilizo hatarini watu 2 kati ya 3 sawa na watu bilioni moja kote duniani hawana sehemu muhimu za kunawa mikono na sabuni na hawana maji nyumbani na nusu yao ni watoto, hali ambayo inaweka hatarini zaidi maisha yao wakati huu wa janga la corona. 

Hivyo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa “Ni lazima tuchukue hatua kuharakisha upatikanaji wa huduma hizi kwa watu wote bila kujali wapi wanakoishi. Sio tu kwa kupambana na janga hili lakini katika kuhakikisha kwamba kila jamii inaweza kupata fursa ya huduma hizi za msingi za kuokoa maisha.”

Amesema hivi sasa UNICEF na wadau wengine wanaongeza kasi ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma za WASH ili kuzisaidia jamii mbalimbali kupambana na COVID-19.

Amependekeza hatua zichukuliwe katika maeneo matatu ili kufanikisha huduma hizo kwa wote ambayo ni ufadhili, takwimu sahihi na ubunifu kwani mazoweya pekee hayatoshi kutatua changamoto hizo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud