COVID-19 inaweza kurudisha nyuma mafanikio yaliyofikiwa kwa miaka hata miongo-Guterres

14 Julai 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo akihutubia hafla ya uzinduzi wa “Mkutano wa juu wa Mawaziri la Siasa kuhusu Maendeleo Endelevu na Mkutano wa ngazi ya juu wa  Baraza la Uchumi na Jamii” ameeleza kuwa janga la COVID-19 linaweza kuyarejesha nyuma maendeleo yaliyofikiwa na  dunia kwa miaka kadhaa na hata miongo kadhaa na kuwa limeleta changamoto kubwa za kiuchumi na ukuaji katika nchi nyingi.

Katibu Mkuu Guterre amesema, “tayari tunakabiliana na changamoto nyingi: kiwango cha juu cha njaa; kuzidi kwa haraka kwa mabadiliko ya tabianchi, kuendelea kukosekana kwa usawa wa kijinsia na pengo kubwa la ufadhili. Hii leo tunakabiliana na changamoto nyingine kubwa ya ulimwengu yaani janga la virusi vya corona ambavyo vitatupeleka mbali na mbali zaidi kutoka kwenye malengo ya maendeleo yetu endelevu.”

Mkutano wa juu wa Siasa kuhusu Maendeleo Endelevu umefanyika kuanzia tarehe 7 hadi 16 mwezi huu wa Julai mwaka 2020 na unajumuisha siku tatu za mikutano ya mawaziri kuanzia leo tarehe 14 ili kufanya mapitio ya njia au hatua za dunia kuelekea kuyafikia malengo 17 ya maendeleo endelevu kufikia mwaka 2030, mafanikio ambayo yameshafikiwa, changamoto, na mafunzo yaliyopatikana.

Rais wa Baraza Kuu la 74 la Umoja wa Mataifa naye akatoa neno

Naye rais wa Baraza Kuu la 74 la Umoja wa Mataifa Tijani Muhammad-Bande akihutubia mkutano huo amee;leza kuwa janga la virusi vya corona limeongeza zaidi kukosekana kwa usawa katika nchi zote. Hatua za kupambana na ugonjwa huo wanazozichukua watu zinapaswa kujikita katika theluthi mbili ya watu wote dunani ambao wanaweza kuachwa nyuma.

Balozi Bande amesema kuwa jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuchukua hatua za pamoja kupunguza madhara kwenye ustawi na maisha ya binadamu katika nchi zinazoendelea.

 “Ili kujikita katika maendeleo baada ya janga la virusi vya corona, lazima tukubali kutekeleza ahadi zetu  za kutoa ufadhili kujitolea kwetu kutoa fedha kwa juhudi endelevu za maendeleo.kwa ajili ya juhudi za kuyafikia maendeleo endelevu.” Amesema Balozi Bande.

Rais wa Baraza la Uchumi

Kwa upande wake rais wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa, Mona Yule amesema kuwa janga la COVID-19 si tu ni tishio kwa afya, lakini pia  janga la mgogoro wa kibinadamu.

Mnamo mwaka 2012, Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu uliamua kuanzisha mkutano kama huu unaofanyika hivi sasa nchi ziutumie kwa hiyari kutoa taarifa kuhusu hatua na mahali walipofikia wakati wa kuelekea kuyafikia maendeleo endelevu. Mwaka huu, nchi au kanda 47 zifanya tathimini au ya kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu yaani SDGs.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud