Burundi yahitaji zaidi ya Rais mpya kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu:UN

14 Julai 2020

Wajumbe wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi leo wamesema taifa hilo la Maziwa Makuu linahitaji zaidi ya kuchagua Rais mpya ili kuweza kukomesha mzunguko wa machafuko unaoambatana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ikiwasilisha ripoti yake mbele Baraza la Haki za binadamu mjini Geneva Uswisi  tume ya umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa haki za binadamu Burundi imesema baada ya kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu Burundi kilichoambatana na visa vya watu kuwekwa rumande na hata kuuawa kwa wajumbe wa chama kikuu cha upinzani nchini Burundi cha CNL, hivi sasa Burundi iko njiapanda.

Na matokeo yake uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge uliofanyika Mei 20 chama tawala CNDD-FDD kimesalia madarakani hivyo mabadiliko pekee ukilinganisha na siku za nyuma ni Rais mpya na jenerali wa zamani Evariste Ndayishimiye.

Kutawala kwa ukiukwaji wa haki za binadamu

Doudou Diene mwenyekiti wa jopo hilo la uchunguzi Burundi amesema “ingawa kwenye uchaguzi huo uliopita hakukuripotiwa machafuko makubwa, mchakato mzima wa uchaguzi ulitawaliwa na hali ya kutovumiliana kisiasa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kabla na wakati wa kampeni rasmi, siku ya uchaguzi na baada ya kutangazwa rasmi kwa matokeo”

Wajumbe wa tume hiyo wamesema wanatambua kwamba katika hotuba yake ya siku ya kuapishwa rais Ndayishimiye alisistiza haja ya kuimarisha hali ya haki za binadamu na kupambana na ukwepaji wa sheria nchini humo lakini pia kushughulikia maridhiano ya kisiasa na kurejea nyumbani kwa wakimbizi wote wa Burundi.

Hata hivyo wajumbe hao wamesisitiza kwamba sera za rais mpya zitatekelezwa na serikali inayoundwa na mzunguko wa Rais aliyetangulia marehemu Pierre Nkurunziza ikiwemo baadhi ya watu ambao wako chini ya vikwazo kwa kujihusisha kwao na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Jopo hilo limetaka ikumbukwe kwamba tangu mwaka 2015 vikosi vya usalama na wajumbe wa muungano wa vijana wa chama tawala ujulikanao kama Imbonerajure umekuwa ukiendesha mauaji ya kiholela, kukamatwa watu kwa nguvu na ubakaji, kutoa vitisho na kuwabughudhi wale waliowachukulia kuwa ni wapinzani wa kisiasa huku wakikwepa sheria.

Wito kwa Rais mpya wa Burundi

Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi Burundi (COIB) imetaka Rais mpya wa Jamhuri ya Burundi kuonyesha utashi wa kuleta mabadiliko kwa kutoa ushirikiano kikamilifu kwa mchakato wa kimataifa wa haki za binadamu ikiwemo COIB, au kwa kuifungua tena ofisi ya umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Burundi.

Wameongeza kuwa kuachiliwa mara moja kwa waandishi wane wa Habari wa Iwacu na watetezi wa haki za binadamu kama Germain Rukuki na Nestor Nibitanga itakuwa ni ishara muhimu sana.

Tume hiyo imekaribisha ukweli kwamba kufuatia kifo cha ghafla cha Rais Nkurunziza 8 Juni 2020, Rais mpya wa Burundi aliamua kushughulikia janga la corona au COVID-19 baada ya miezi kadhaa ya kukana kuwepo kwa ugonjwa huo.

Hata hivyo wajumbe wa tume hiyo wameionya jumuiya ya kitamatifa dhidi ya kulegeza uzi mapema na kubadili ukurasa “kana kwamba uchaguzi na mabadiliko ya kiasa yanatosha kuhakikisha moja kwa moja uboreshaji wa hali ya haki za binadamu katika kusonga mbele.”

Wameongeza kuwa mfumo wa serikali umewekwa kufaidisha CNDD-FDD bado upo. “Mabadiliko haya yanaweza kuwa ni fursa ya kuboresha endapo serikali itachukua hatua muafaka kuzishughulikia. Jumuiya ya kimataifa lazima isalie kuwa makini na kujipanga kuchagiza hatua ambazo zinashughulikia mizizi ya ukiukwaji wa haki za binadamu.” amesisitiza mwenyekiti wa tume Doudou Diène.

Hivi sasa COIB ndio chombo pekee cha kimataifa kinachoendesha uchunguzi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu Burundi. Ingawa serikali haijawahi kuwapa wachunguzi fursa ya kuingia nchini humo wamekuwa wakikusanya taarifa kutoka kwa vuanzo mbalimbali, vya ndani ya nchi na nje.

Tume hiyo itawasilisha ripoti yake ya mwisho kwenye Baraza la Haki za binadamu Septemba 2020.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud