IFAD na kampuni ya Mars zachukua hatua kunusuru wakulima wa kakao na walaji wa chokoleti
IFAD na kampuni ya Mars zachukua hatua kunusuru wakulima wa kakao na walaji wa chokoleti
Mfuko wa kimataifa wa ufadhili wa ajili ya kilimo IFAD na kampuni kubwa ya kutengeneza chokoleti duniani Mars zimeshikamana kuchukua hatua kukabiliana na uhaba wa zao la kakao ambalo ni kiungo muhimu katika utengenezaji wa kiburudisho kinachopendwa kila kona ya dunia, chokoleti.
Chokoleti moja ya viburudisho vinavyopendwa na watu wengi duniani zinapatikana katika maumbo na mchanganyiko wa kila aina lakini ili ziendelee kutengenezwa zinahitaji kiungo muhimu ambacho ni zao la kakao.
Kwa mujibu wa IFAD muongo mmoja uliopita ilitabiriwa kwamba mwaka huu wa 2020 dunia itashuhudia upungufu wa tani milioni moja za kakao kwa mwaka hali ambayo itaathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa zao la kakao na hatimaye utengenezaji wa chokoleti.
Sababu kubwa ya upungufu huo imeelezwa kuwa ni magonjwa na wadudu wanaoshambulia kakao.
Ili kukabiliana na mtihani huo IFAD na wadau ikiwemo kampuni ya chokoleti ya Mars wameanzisha mradi wa kuwapa mafunzo wakulima wadogowadogo ili wawe madaktari wa kakao, mafunzo ambayo yataboresha afya ya zao la kakao lakini pia matarajio ya kiuchumi kwa wakulima na viwanda vya chokoleti duniani.
Kutana na Ahmmed mmoja wa madaktari wa kwanza kabisa wa kakao, yuko Sulawesi Indonesia nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji wa zao la kakao, maisha yake yote amekuwa mkulima wa kakao lakini sasa alianza kupoteza matumaini kutokana na magonjwa na wadudu wanaoshambulia zao hilo “Wakati mwingine ninakata tamaa ya kufanya kazi ya bila faida, nitaendeleaje kulima kama sina fedha, wakati mwingine nachanganyikiwa kabisa hadi kichwa kinaniuma na hata ninalia nikiwa nyumbani , nitatatuaje changamoto hii.”
Lakini baada ya IFAD, serikali ya Indonesia na kampuni ya Mars kufungua kituo cha mafunzo kwa wakulima Ahmmmed alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufundishwa ili naye akafundishe wakulima wengine
“Sasa moyo wangu umejawa na furaha namshukuru mungu nimeushinda mtihani huu ntaendelea kufanya bidii katika kilimo cha kakao kwa sababu ndio kitu pekee kitakachoboresha pato la maisha yangu.”
Maelfu ya wakulima wa kakao wameshafaidika na mafunzo hayo ambayo si faraja kwao na familia zao tu bali pia kwa wazalishaji na walaji wa chokoleti kote duniani.