Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na Wizara ya afya Sudan Kusini washughulikia unyanyapaa unaowakumba hadi wanaompana na COVID-19

Wananchi wa Sudan Kusini katika soko la Konyo Konyo mjini Juba wakijisomea taarifa kuhusu COVID-19 baada ya kupatiwa barakoa za kitambaa.
© UNICEF/Bullen Chol
Wananchi wa Sudan Kusini katika soko la Konyo Konyo mjini Juba wakijisomea taarifa kuhusu COVID-19 baada ya kupatiwa barakoa za kitambaa.

WHO na Wizara ya afya Sudan Kusini washughulikia unyanyapaa unaowakumba hadi wanaompana na COVID-19

Afya

Unyanyapaa unaotokana na uoga ni moja ya vikwazo katika kudhibiti janga la COVID-19 na vimeshuhudiwa na wanajamii na pia wafanyakazi na mamlaka wanaopambana na COVID-19 nchini Sudan Kusini, inaeleza taarifa iliyotolewa hii leo mjini Juba na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO.

Kabla ya Sudan Kusini kutangaza mgonjwa wa kwanza wa COVID-19, ujumbe wa kujikinga ulikuwa kila mahali. Watu wengi walikuwa na wasiwasi wakati walipohimizwa waache kusalimiana kwa kushikana mikono na pia wakiambiwa wazingatie umbali kati ya mtu na mtu ingawa maisha ya watu wa Sudan Kusini yanaegemea sana katika mwingiliano wa kijamii.

Mgonjwa wa kwanza aligundulika mwezi Aprili mwaka 2020 kisha kusambaa kwa virusi vya corona kukachochea wasiwasi mwingine: watu si tu kuwa waliuogopa ugonjwa, pia waliogopa namba watakavyochukuliwa na watu wao wa karibu katika familia, ndugu na majirani ikiwa watapata ugonjwa wa COVID-19. Wengine, hata wanaotambua hatari ya ugonjwa, waliogopa kwenda kupima.

Mathew Tut Mkurugenzi wa Kituo cha afya ya umma na dharura cha Sudan Kusini aliambukizwa virusi vya corona wiki chache tu baada ya virusi hivyo kugundulika nchini humo. Pamoja na kuikubali hali yake nma kujitenga mwenyewe kwa kukaa mbali na marafiki zake na familia yake, alijisikia kutengwa kijamii na anasema, “nilijihisi kuwa watu wangu wa karibu ambao wangenisaidia na kunipa moyo katika nyakati ngumu kama hizo, walinitelekeka. Hali yote hiyo ilinipa mawazo mageni, nilishangaa kwa nini watu walikuwa wanikwepa kama vile ghafla nimekuwa mtu mbaya. Zilikuwa nyakati ngumu za maisha yangu.”

Kuhusu unyanyapaa, Tut analaumu kukosekana kawa taarifa za kutosha kuhusu janga hili hususani uelewa mdogo wa watu kuhusu namna ugonjwa huu unavyoambukiza na namna wanavyoweza kuushughulikia baada ya kupata maambukizi. Tut anasisitiza kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kuwahamasisha watu kuuliza maswali na kutafuta ufafanuzi zaidi.

Mtu mwingine miongoni mwa wengine aliyekumbwa na unyanyapaa ni James Ayei. Kwa kufahamika katika maeneo yake kuwa anafanya kazi katika kikosi cha wanaopambana na COVID-19, mwanasayansi huyo mwenye utaalamu wa vimelea vya magonjwa alianza kuangaliwa kwa jicho la tahadhari.

“Wakati mgonjwa wa kwanza alipodhibitika Sudan Kusini, kila mtu katika mtaa wangu alifahamu kuwa nilikuwa miongoni mwa timu ya watu wanaopima sampuli zilizokusanywa kote nchini kwa kuhisiwa kuwa na COVID-19. Mimi ni binadamu. Ni mtaalamu wa vimelea vya magonjwa na hicho ndicho ninachokifanya ili kuishi. Wnachopaswa kufahamu ni kuwa COVID-19 ni virusi na vinaweza kumwambukiz kila mtu awe ni mtu anayefanya kazi katika sekta ya afya au nje ya hapo.”

Kushughulikia suala la unyanyapaa

Kwa kuwa unyanyapaa unaweza kuzuia hatua za kupunguza maambuki ya COVID-19, na kusababisha watu kujificha kwa kuogopa kubaguliwa na hivyo kuwafanya kutotafuta tiba kwa haraka na pia kutofuata masharti kama kuvaa barakoa, WHO nchini Sudan Kusini na Wizara ya afya ya nchi hiyo, wanashirikiana kikamilifu katika kutoa mwongozo wa kushughulikia suala la unyanyapaa, mwongozo ambao unajumuishwa pia kama sehemu ya mafunzo kwa wahudumu wa afya na wale wanaojitolea. Ujumbe pia unapelekwa kwa umma. Juhudi zinafanyika pia ili kujenga imani   na kushughulikia suala la hofu na taarifa za uongo.