Mwelekeo wa COVID-19 kwa nchi nyingi uko kisegemnege – Dkt. Tedros

13 Julai 2020

Shirika la afya la  Umoja wa Mataifa , WHO limesema kuwa mataifa mengi zaidi yana mwelekeo usio sahihi katika kupambana na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesisitiza kuwa mwelekeo huo usio sahihi sambamba na kauli mkanganyiko kutoka kwa viongozi vinatowesha kiambato muhimu zaidi cha kutokomeza COVID-19, ambacho ni imani.
“Virusi hivi vimesalia kuwa adui namba mmoja wa umma, lakini hatua za serikali nyingi na watu wake haziakisi hali hii. Lengo kuu la virusi ni kupata watu na kuwaambukiza,” amesema Dkt. Tedros.
Amesisitiza kuwa, “iwapo mambo ya msingi hayafuatwi, kuna njia moja ambayo janga hili itafuata. Hali itakuwa mbaya, mbaya na mbaya. Lakini haipaswi kuwa hivi. Kila kiongozi, kila serikali na kila mtu anaweza kuchukua hatua kuvunja mnyororo wa maambukizi na kutokomeza machungu ya sasa.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema kuwa hakuna njia ya mkato kutokomeza janga la COVID-19, akiongeza kuwa, “tunatumai kutakuwepo na njia fanisi ambayo ni chanjo, lakini sasa hivi tunapaswa kujikita katika kutumia mbinu zilizopo kutokomeza maambukizi na kuokoa maisha. Tunapaswa kufikia hali endelevu ambayo kwayo tuna udhibiti wa kutosha wa virusi bila kuweka udhibiti wa maisha yetu.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa WHO anayehusika na mipango ya dharura za kiafya, Dkt. Michael Ryan amesema kuwa, “iwapo watu wataendelea kumiminika kwenye maeneo yenye umati mkubwa bila kuchukua hadhari kama vile kuvaa barakoa na kuepuka kuchangamana, basi huu ugonjwa utaendelea kusambaa.”

 

Takwimu za COVID-19

Hadi leo Julai 13, 2020, takwimu za WHO zinaonesha kuwa jumla ya watu 12,768,307 duniani kote wameambukizwa virusi vya Corona na kati yao hao 566,654 wamefariki dunia. 

Idadi ya maambukizi mapya kwa siku yaongezeka Marekani.

Ukanda unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na vifo ni Amerika ambao una wagonjwa 6,669,879.
Katika ukanda huo wa Amerika, Marekani inashika nafasi ya kwanza ambapo tarehe 1 mwezi huu wa Julai wagonjwa zaidi ya 35,000 walithibishwa kwa siku moja na hii leo idadi ya wagonjwa wapya kwa siku moja moja ni zaidi ya elfu 65.
Brazil inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ukanda wa Amerika.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter