Makubaliano ya kuvusha misaada kwenda Syria yakifikia ukomo, Baraza la Usalama linachemsha bongo

10 Julai 2020

Leo Julai 10 ndiyo siku ya ukomo wa azimio namba 2504 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloidhinisha makubaliano ya shughuli za kuvusha misaada ya kibinadamu kupitia mpaka wa Uturuki kuingia Syria. Kutokana na umuhimu wa misaada hiyo, hali hiyo inaweka shinikizo kubwa kwa Baraza la Usalama kutafuta namna ya kuongeza muda zaidi wa uvushaji misaada ili kuokoa maisha ya watu. 

Katika eneo la Reyhanli kwenye mpaka wa Uturuki na Syria, Magari kwa muda sasa yamekuwa yakivusha misaada ambayo kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu, OCHA, ni misaada ya muhimu kwa maisha ya watu milioni 2.8, wanaume, watoto kwa wanaume ambao wanahitaji misaada ya kibinadamu kote kaskazini magharibi mwa Syria.

UNOCHA
Watoto wakiwa nje ya hema katika kambi ya watu waliotawanywa huko Idlib, kaskazini mwa Syria.

 

OCHA inasema wakati operesheni za hizi za kuvusha misaada kutoka upande wa Uturuki kuingia Syria zikiwa zimepangwa kufikia ukomo hii leo Julai 10, hivi sasa hakuna njia mbadala ambayo inaweza kufanana kwa kiwango na mawanda operesheni hiyo ambayo inaendelea kujibu mahitaji mazito ya mamilioni ya raia.

Kwa mjibu wa OCHA, mwezi uliopita yaani Juni takribani lori 1,759 zilivuka mpaka na kusambaza msaada wa kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni 6 wakati kwa mwezi mmoja zaidi nyuma yaani mwezi Mei, ilirekodiwa idadi kubwa zaidi ya lori za msaada wa kibinadamu za Umoja wa Mataifa zinazovuka kila mwezi tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo mnamo mwaka 2014 ambapo zilivuka lori 1,781 kwa mwezi huo pekee.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud