Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wimbo maarufu One Love wa Bob Marley kutengenezwa upya ili kuiunga mkono 'Reimagine' ya UNICEF

Msanii na mwanamuziki wa mtindo wa reggae Ziggy Marley alipoahidi kuunga mkono kampeni ya 'Sema ndio kwa watoto' alipotembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Julai 2001
© UNICEF/Nicole Toutounji
Msanii na mwanamuziki wa mtindo wa reggae Ziggy Marley alipoahidi kuunga mkono kampeni ya 'Sema ndio kwa watoto' alipotembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Julai 2001

Wimbo maarufu One Love wa Bob Marley kutengenezwa upya ili kuiunga mkono 'Reimagine' ya UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Wanafamilia wa mwanamuziki nguli na wa kukumbukwa sana duniani, Bob Marley, wametangaza kuutengeneza upya wimbo maarufu wa Bob Marley unaofahamika kwa jina One Love ili waunge mkono kazi za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF, kurejesha tena ulimwengu wa haki zaidi kwa watoto ambao maisha yao yamevurugwa na janga la COVID-19, imeeleza taarifa ya UNICEF iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani.

Kampuni ya Tuff Gong International na Amplified Music watatoa toleo jipya la wimbo huo wa One Love tarehe 17 mwezi huu wa Julai. Mapato yote kutoka katika wimbo hu una shughuli zote kuhusu jambo hili, yatasaidia moja kwa moja kampeni ya UNICEF iliyopewa jina Reimagine ikilenga kuzuia COVID-19 kuwa janga la kudumu kwa watoto na kuhakikisha ulimwengu baada ya janga hili unakuwa bora zaidi na sawa kwa kila mtoto.

Kuanzia leo kampuni ya vito ya Pandora ambayo ni mdau wa kimataifa wa UNICEF itahusisha kila dola itakayochangwa na umma kwenda One Love hadi kufikia kisi cha dola milioni 1 za kimarekani.

Mtoto wa kike wa Bob Marley, Cedella Marley amesema, “kwa zaidi ya miaka 40, baba yangu aliandika One Love kuhusu umoja, amani na upendo wa pamoja wa ulimwengu wakati ambapo kulikuwa na shida nyingi duniani. Hata katika nyakati amabzo hatuwezi kuwa pamoja, ujumbe wake unasalia kuwa kweli leo. Tunaweza kulipita janga hili la ulimwengu ikiwa tutakuja pamoja kupitia upendo mmoja na moyo mmoja.”

Ni wimbo wenye ujumbe hai kwa miaka yote

Bob Marley akiwa na kundi la the Wailers, waliurekodi wimbo wa One Love mwaka 1977 na tangu wakati huo umesalia kuwa na ujumbe wake unaobakia kuwa hai wakati wote ukiwasihi watu kuwa kuja pamoja na kuwa kitu kimoja.

Taarifa ya UNICEF imesema, “toleo hili jipya la wimbo huu litakuwa wimbo wa kweli wa ulimwengu  katika mwaka huu wa 2020 ukiwajumuisha wana familia ya Bob Marley, wanamuziki wakubwa kutoka kila pembe ya dunia, wasanii kutoka katika maeneo yenye mizozo duniani kote na watoto wanaoishi katika jamii zilizoko hatarini.upya la wimbo huo litakuwa wimbo wa kweli wa ulimwengu kwa mwaka 2020 wenye washiriki wa familia ya Marley, walianzisha wanamuziki kutoka pembe zote za ulimwengu, wasanii kutoka maeneo ya migogoro kote ulimwenguni, na watoto wanaoishi katika jamii zilizo hatarini.”

Tunaishukuru familia ya Bob Marley

Naye Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Bi Henrietta Fore amesema, “wimbo wa One Love unaongea moja kwa moja kwenye ukweli muhimu kuhusu janga hili: Tumaini letu bora kuishinda COVID-19 na kurejesha ulimwengu sawa, usio na ubaguzi kwa watoto ni kupitia  mshikamano na ushirikiano wa  kimataifa. Tunafurahi kuwa familia ya Marley pamoja na Pandora wametoa msaada wao, ubunifu na upendo ili kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi.”

UNICEF inakadiria kuwa nyongeza ya watoto 6,000 katika miezi sita ijayo, wanaweza kufariki kila siku kutokana na sababu zinazozuilika na karibia wote yaani zaidi ya asilimia 90 wako katika ncho za kipato cha chini na cha kati, kwa kuwa janga linaendelea lkudhoofisha mifumo ya kiafya na kuvuruga huduma.  

Ili kusaidia uzinduzi wa toleo jipya la wimbo wa One Love, huduma ya mtandao wa TikTok itakuwa na tukio maalumu na shindano kwa mashabiki katika kipindi ambacho wimbo utakuwa unazinduliwa. Taarifa nyingine kuhusiana na wimbo huu zitatolewa katika siku zijazo.