Ukata na COVID-19 vyaweka njiapanda maisha ya wakimbizi Afrika:UNHCR/WFP

9 Julai 2020

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la mpango wa chakula duniani WFP yameonya kwamba ukata wa ufadhili, vita, majanga, changamoto za usambazaji misaada, ongezeko la bei ya vyakula na kupoteza kipato kutokana na janga la corona au COVID-19 vinatishia kuwaacha mamilioni ya wakimbizi barani Afrika bila chakula.

Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis na mashirika hayo mawili, kamishina mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi amesema “Mamilioni ya wakimbizi barani Afrika hivi sasa wanategemea msaada wa kila siku kuweza kukidhi mahitaji yao ya chakula na karibu nusu ya wakimbizi hao ni watoto ambao wanaweza kupata matatizo ya muda mrefu kiakili na kiafya kwa kukosa lishe bora katika hatua muhimu ya ukuaji wao katika maisha.”

Ameongeza kuwa endapo hatua hazitochukuliwa sasa kushughulikia hali hiyo basi viwango vya utapiamlo uliokithiri, kudumaa na upungufu wa damu au anemia vinatarajiwa kuongezeka.

Kwa mfano amesema katika makambi ya wakimbizi nchini Ethiopia asilimia 62 ya watoto wanakabiliwa na matatizo ya kiwango cha juu cha anemia.

Naye mkrugenzi mtendaji wa WFP David Beasely amesisitiza kwamba “wakati hali inaendelea kuzorota kila mahali janga linaongezeka kwa wakimbizi ambao hawana chochote. Na janga la corona limeongeza wasiwasi hususan kwa wale wanaotegemea misaada pekee ili kuishi. Sasa kuliko wakati mwingine wowote wanahitaji msaada wetu ili kuishi na kuokoa maisha yao.”

WFP inatoa msaada wa chakula kwa wakimbizi zaidi ya milioni 10 duniani kote ikiwemo katika makazi makubwa kabisa ya wakimbizi ya Bidibidi nchini Uganda ambayo mwezi Aprili mwaka huu yalishuhudia mgao wa chakula ukipunguzwa kwa asilimia 30 kutokana na ukata.

Hivi sasa wakimbizi wengi wamepoteza pato kutokana na COVID-19 na vikwazo vya usafiri vimezidisha changamoto za ugawaji misaada.

Jumla ya wakimbizi milioni 3.2 Afrika Mashariki wamepunguziwa mgao wa chakula kutokana na ukata ikiwemo Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini na Tanzania, pia mgao umepunguzwa katika nchi za Malawi, DRC, Msumbiji na Zambia.

UNHCR na WFP kwa pamoja wanahitaji jumla ya dola milioni 921 ili kuwasaidia wakimbizi wa Afrika pekee katika miezi sita ijayo.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter