Tumepokea notisi ya Marekani kujitoa WHO ifikapo 2021- UN

7 Julai 2020

Umoja wa Mataifa umesema umepokea taarifa ya serikali ya Marekani ya kujitoa rasmi kwenye shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO.
 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric kupitia taarifa yake kwa waandishi wa habari hii leo, amesema kuwa, “kwa jibu la maswali ambayo nimepokea hivi sasa, naweza kusema kuwa tarehe 6 Julai mwaka 2020, Marekani ilimjulisha Katibu Mkuu, kwa nafasi yake ya mhifadhi wa Katiba ya WHO juu ya kujitoa kwake kwenye shirika hilo kuanzia tarehe 6 mwezi Julai mwaka 2021.”

Mchakato unaendelea kuona kama Marekani imekidhi masharti ya kujitoa WHO

Bwana Dujarric amesema kuwa Marekani ni mwanachama wa WHO tangu tarehe 21 mwezi Juni mwaka 1948 na “ushiriki wa Marekani ulikubaliwa na Baraza Kuu la WHO kwa masharti kadhaa yaliyowekwa iwapo Marekani itajitoa WHO. Masharti hayo ni pamoja na kutoa notisi ya mwaka mmoja na kumaliza malipo yake yote kwa mujibu wa wajibu wake kifedha.”

Msemaji huyo ametamatisha taarifa yake akisema kuwa, “Katibu Mkuu, kwa nafasi yake ya mhifadhi,  yuko katika mchakato wa kuthibitisha ndani ya WHO iwapo masharti hayo yametimizwa ili hatua ya kujiondoa iweze kutekelezwa.”

Takribani miezi miwili iliyopita, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza nia yake ya kuondoa Marekani kwenye shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa, hadi baada ya tathmini ya hatua za shirika hilo dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

COVID-19 hadi leo

Kwa mujibu wa WHO hadi leo Julai 7, 2020,  ugonjwa wa Corona umethibitishwa kwa watu 11,500,302 ulimwenguni ambapo kati yao hao 535,759 wamefariki dunia, ukanda wa Amerika ukiongoza ukifuatiwa na Ulaya.
Nchini Marekani, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa ni 2,877,238 na kati yao hao 129,643 wamefariki dunia, Marekani ikiwa inaongoza sasa kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na vifo duniani.

Ifahamu WHO

WHO ilianza kazi yake tarehe 7 mwezi Aprili mwaka 1948 wakati ambapo Katiba yake ilipokamilika, tarehe ambayo hivi sasa inatambuliwa kuwa ni siku ya afya duniani.

Ikiwa na makao yake makuu mjini Geneva, Uswisi na ofisi 6 za kikanda ikiwemo Afrika, WHO yenye nchi wanachama 194, ina jukumu kuu la kuongeoza na kuratibu afya duniani kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Maeneo ya kazi ni mifumo ya afya, afya ya binadamu, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, kuijandaa dhidi ya magonjwa, kusimamia na kuchukua hatua na huduma za kishirika.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter