Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wakenya wasio na uhakika wa chakula kuongezeka mara mbili mwaka huu:WFP

Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa  jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote
Picha-IFAD
Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote

Idadi ya wakenya wasio na uhakika wa chakula kuongezeka mara mbili mwaka huu:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limeonya kwamba idadi ya wakenya wasio na uhakika wa chakula na kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu sasa kuongezeka zaidi ya mara mbili mwaka huu .

Kwa mujibu wa taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, mwishoni mwa mwaka 2019 kulikuwa na Wakenya milioni 1.3 walioathirikavibaya na ukosefu wa chakula lakini sasa shirika hilo  inasema mwezi huu wa Julai idadi inatarajiwa kuongezeka na kufikia kati ya milioni 3 hadi milioni 3.5 wakati familia zitakapoishiwa kabisa chakula msimu wa muambo utakapofikia kilele.

Kwa kusaidia juhudi za serikali ya Kenya ambayo kwa sasa inapambana na janga la corona au COVID-19 WFP “inatoa msaada wa fedha taslim za miezi mitatu kwa watu 279,000 wanaoishi katika makazi yasiyorasmi mjini Nairobi kwa familia ambazo tayari zilikuwa zinahaha kujilisha hata kabla ya janga la corona.”

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao mjini Geneva msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema wanazisaidia pia familia zingine 70,500 ambazo kipato chake kimepunguzwa au kimetoweka kutokana na COVID-19 “WFP itatoa shilingi 4,000 za Kenya kila mwezi sawa na dola 40 kupitia utaratibu wa M-pesa kwa kila kaya ambayo inastahili ili kufidia karibu nusu ya gharama za chakula kwa wastani wa familia ya watu wane kulingana na mwongozo wa programu ya serikali ya msaada wa fedha .

Ameongeza kuwa uhakika wa chakula na lishe wa watu hao umesambaratishwa na janga la COVID-19 na kuwafanya watu masikini wa mijini sasa kutumia karibu nusu ya pato lao kwa chakula.

Kwa kushirikiana na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na wizara ya afya ya Kenya, WFP pia itatoa msada wa chakula cha kutibu watoto wa chini ya miaka mitano 16,000 walio na utapiamlo uliopindukia, kina mama wajawazito na wanaonyonyesha 5,700 na wazee 6,800  ambao wanaishi kwenye makazi duni.

Ili kufanikisha hilo WFP inahitaji dola milioni 33.9 kuhakikisha chakula na lishe sio tu raia wa Nairobi kwenye makazi yasiyorasmi bali kupanua wigo wa msaada kwa maeneo mengine kama Mombasa, Nakuru, Kilifi na Kwale.