Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yadhihirisha udhaifu dhidi ya aina mpya za ugaidi:Guterres

Kama sehemu ya kampeni kuhusu COVID-19, kamanda wa Bangladesh anayehudumu katika MINUSCA nchini CAR akimhamasisha mkandarasi mwenyeji kuvaa barakoa.
MINUSCA
Kama sehemu ya kampeni kuhusu COVID-19, kamanda wa Bangladesh anayehudumu katika MINUSCA nchini CAR akimhamasisha mkandarasi mwenyeji kuvaa barakoa.

COVID-19 yadhihirisha udhaifu dhidi ya aina mpya za ugaidi:Guterres

Amani na Usalama

Janga la corona au COVID-19 limedhihirisha udhaifu uliopo kwa aina mpya za zinazoibuka za mifumo ya ugaidi, ameonya leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitolea mfano matumizi mabaya ya teknolojia ya kidijitali, mashambulizi ya kupitia mtandao na mashambulizi ya makusudi ya kutumia virusi, bakteria au vijidudu vingine vinavyoweza kusababisha maradhi.

Antonio Guterres akizungumza kwa njia ya mtandao kwenye ufunguzi wa mkutano wa wiki ya Umoja wa Msataifa kupinga ugaidi amesema “Kama vilivyo virusi vya corona, ugaidi hauheshimu mipaka ya kitaifa, unaathiri mataifa yote na tunaweza kuushinda tu kwa juhudi za pamoja.”

Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi na mashirika ya kimataifa kukumbatia uwezo wa mshikamano wa kimataifa katika janga hili la kimataifa linalobadilika kila uchao.

Guterres amesema ingawa ni mapema mno kufanya tathimini kamili ya athari za COVID-19 katika masuala ya ugaidi, ameonya kwamba mashirika ya kigaidi lama ISIL na Al-Qaeida, lakini pia Unazi mamboleo na makundi ya waodhani wazungu ni bora Zaidi ya wengine , wanajaribu kuleta mgawanyiko na kuutumia, kusababisha migogoro, utawala mbovu na machungu waliyonayo watu ili kusongesha mbele malengo yao wakati huu wa janga la corona.

Hatua tano za kudhibiti ugaidi

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaamini kwamba vita dhidi ya ugaidi vinahusisha hatua tano muhimu ambazo ni:

  1. Kuwekeza katika uwezo na njia ambazo zinaweza kukabiliana na vitisho vya ugaidi
  2. Kuwa na teknolojia ya kuweza kuwafuatilia magaidi na kuwasambaratisha
  3. Kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa
  4. Kutoruhusu magaidi kutumia upenyo wowote ulioletwa na janga la corona
  5. Na kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa na uzoefu.

Bwana. Guterres ametoa wito kwamba “Katika zama hizi za corona natoa wito kwa mataifa yote kujizatiti wenyewe kufanya juhudi Zaidi na kwa ufanisi katika mapambano dhidi ya ugaidi. Kama katika maeneo mengine ya wajibu wetu , kazi yetu lazima itathiminiwe kwa mabadiliko tunayoleta katika Maisha ya watu.”

Amekumbusha kwamba vita imara dhidi ya ugaidi haviwezi kufanyika kwa kuweka rehani maadili yetu ya Pamoja kwenye Umoja wa Mataifa.