UNESCO yaonya dhidi ya hati za kughushi zinazodai kuidhinisha usafirishaji wa sanaa za kitamaduni za Kiafrika

1 Julai 2020

UNESCO, kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo mjini Paris Ufaransa, inahimiza uangalifu mkubwa baada ya kupokea ripoti nyingi za udanganyifu na usafirishaji haramu wa mali za kitamaduni za Kiafrika kwa kutumia nyaraka za uongo zikidai kuwa UNESCO inathibitisha biashara kama hiyo na hata kuthibitisha thamani ya bidhaa hizo.

Nyaraka hizo za kugushi, kwa njia ya uongo zinakuwa na jina na nembo ya UNESCO, na wakati hutumia kadi bandi za anwani na mawasiliano zenye majina ya maafisa wa UNESCO.

“Wengi wa waathirika wa ulaghai huu wanaishi Ufaransa, wengi wanaweza kuwa na  uhusiano na nchi za kiafrika zinazozungumza Kifaransa na wanaamini wana uelewa kuhusu mambo yanayoendelea. Makadirio ya hasara yanafikia zaidi ya euro milioni moja.” Imeeleza taarifa hiyo

UNESCO imesema inafikiria kuchukua hatua za kisheria ili kutokomeza ulaghai huu pamoja na matendo yanayochafua jina lake.

Shirika hilo limetoa wito kwa watu wote ambao wanapokea bidhaa hizo, "kufanya umakini mkubwa na uhakiki wa kina kuhusu uhalali wa bidhaa hizo kabla ya kujihusisha nazo. Aidha shirika hilo limetoa wito kwa watu wanaopata bidhaa hizo zenye hati ghushi, kutoa taarifa kwa mamlaka za kisheria."

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay amesema, “usafirishaji haramu wa mali za kitamaduni ni janga kubwa la ulimwengu ambalo mara nyingi lina uhusiano na aina nyingine za uhalifu wa kupangwa ikiwemo ufadhili wa ugaidi. Linaathiri maeneo yote ya dunia, hususani bara la Afrika. Matendo haya maovu yanaumiz utamaduni.”

Naye Ernest Ottone Ramirez ambaye ni Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa utamaduni wa UNESCO, ameongeza kwa kusema kuwa hivi sasa si tu Afrika ambayo urithi wa utamaduni wake kwa muda mrefu umekuwa mwathirika wa wizi na uharibifu, lakini pia hli hiyo hivi karibuni inatokea Mashariki ya kati ikihusianishwa na migogoro nchini Iraq na Syria. Aidha inakua zaidi katika intaneti ambako kufuatilia asili ya bidhaa fulani na wahusika ni vigumu.

Mwaka huu UNESCO inaadhimisha miaka 50 ya Mkataba uliopitishwa mnamo mwaka 1970 wa kupambana na usafirishaji haramu wa mali za kitamaduni.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter