Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati Madhubuti wahitajika kuurejesha uchumi ulioathirika na COVID-19 katika mstari:UN

Mama mmoja akiwa kazini na binti wake wawili akifanya kazi kama muuzaji wa matunda huko Dhaka, Bangladesh.
UN Women/Fahad Abdullah Kaizer
Mama mmoja akiwa kazini na binti wake wawili akifanya kazi kama muuzaji wa matunda huko Dhaka, Bangladesh.

Mkakati Madhubuti wahitajika kuurejesha uchumi ulioathirika na COVID-19 katika mstari:UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ametoa wito wa mawazo na mkakati Madhubuti ili kuurejesha uchumi wa dunia ulioathirika na janga la Corona au COVID-19 katika mstitari na kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katika taarifa yake kwenye mjadiliano maalum yaliyofanyika kwa njia ya mtandao Guterres ameonya kwamba “Endapo hatutochukua hatua sasa tunaweza kukabilia na miaka ya kudorora na kutokua kwa uchumi. Janga hili linatishia kusitisha ajenda ya maendeleo ya 2030 lakini pia kubadili hatua ambazo tayari zimeshapigwa kufikia maendelep hayo. Nimekuwa nikitoa wito wa kuwa na mingo mahsusi tangu mwanzo wa janga hili.”

Katika mjadala huo ambao umehudhuriwa pia na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed na waziri wa fedha wa Indonesia Sri Mulyani Inrawati, Katibu Mkuu ameongeza kuwa nchi zilizoendelea zimetekeleleza mkakati wa kuokoa uchumi kwa kutumia rasilimali zake au kwa kuchapisha fedha lakini “Tatizo ni kuhakikisha kwamba nchi zinazoendelea zina rasilimali au zinapokea rasilimali ili kuweza kuwa na mipango saw ana hiyo kuokoa chumi zake”

Maendeleo na changamoto ya ufadhili

Katika suala la maendeleo na ufadhili Guterres anafikiria suluhu ambazo ni za lazima, imara na za mabadiliko yanayoweza kufikia na anatumai kwamba mlolongo wa majadiliano haya unaweza kuleta mawazo mapya.

“Ni janga la kibinadamu, lakini sasa limekuwa la maendeleo na ufadhili, endapo nchi hazitokuwa na uwezo wa kifedha kupambana na janga hili na kuwekeza katika kujikwamua kiuchumi tutakabiliwa na zahma ya kiafya na machungu ya ukuaji wa polepole sana wa kiuchumi.”

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu kusambaa kwa mgogoro wa madeni kunatishia nchi nyingi kujikuta njia panda kuchagua ama kuhudumia madeni, kulinda watu wake walio hatarini katika jamii na kupambana na janga hili.

“Ni lazima tutatue tatizo la madeni kwa nchi zinazoendelea na kwa idadi kubwa ya nchi zilizo na kipato cha wastani ambazo zimepoteza uwezo wa fursa za kufikia masoko ya fedha. Pia tunapaswa kuanza kufikiria kuhusu suluhu ya madeni endelevu ambayo yatatoa mwanya wa uwekezaji katika kujikwamua na malengo ya maendeleo endelevu”, amesema Guterres na kuongeza kuwa hali ya sintofahamu na sera za kujilinda kutasababisha muda mrefu wa ufadhili mdogo wan je na wakati janga la COVID-19 likivuruga mnyororo wa usambazaji na biashara kuna hatari kwamba baadhi ya sekta za viwanda zikarejea kwa nchi zilizoendelea na hivyo kupunguza Zaidi rasilimali katika nchi zinazoendelea na kuzusha maswali kuhusu ujumuishwaji wa wao katika uchumi wa dunia. “Maswali haya yanahitaji majibu muafaka na bunifu” amehitisha Katibu Mkuu katika taarifa yake.

Mabadiliko makubwa yanahitajika

Naye Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed akiongeza sauti yake katika majadiliano hayo amesema “Katika kuutafakari uchumi mpya wa dunia ambao ufadhili wa fedha unakuwa ndio njia na sio mwisho, basi ufadhili wa fedha toka nje unahitaji kubadili mwelekeo. Tunahitaji ushirika na masoko ya fedhaili kubadili uwiano uliopo na kufikia SDGs. Hivyo uwekezaji hauwezi tu kuwa sababu ya faida kwa gharama yoyote bali lazima utue katika upande sahihi wa historia.”

Bi. Mohammed amesisitiza kwamba “ Mabadiliko lazima yazibe pengo la usawa na mmomonyoko wa mazingitara ambao unaweka wingu nene katika mustakbali wetu . Lazima kuwe na uchumi mpya wa kimataifa ambao msingi wake ni matumizi na uzalishaji endelevu na wenye miundombinu endelevu ambayo inatoa fursa kwa wote kwa ajili ya fursa za siku za usoni na tunahitaji kufanya hivyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.” Amehitimisha Naibu Katibu Mkuu na kuongeza kuwa “Kuzaliwa upya kwa uchumi wa dunia ni fursa ya kuwawezesha kukabiliana na hali sasa na changamoto zijazo.”