Michoro na picha vyasaidia wakuchi kuelewa jinsi ya kujikinga na Corona

1 Julai 2020

Nchini Afghanistan,  hatua za kuzuia watu kuchangamana kwa lengo la kuepusha kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, zimesababisha watu wapatao milioni 1.5 nchini humo kukabiliwa na njaa na ugumu wa maisha.
 

Miongoni mwao ni wafugaji wa kuhamahama wa jamii ya wakuchi ambao kwa miezi mitatu iiyopita, wamesalia na kipato kidogo na kiasi kidogo cha chakula.

Mfuko wa maendeleo ya kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD unasema kuwa kufungwa kwa masoko makuu kumebakiza maeneo machache ya kufanya biashara kwa lengo la kupata kipato huku mipaka ikiwa imefungwa na bei za bidhaa muhimu kama vile sukari na mchele zikiongezeka mara tatu.

Wakuchi ni miongoni mwa makabila masikini zaidi nchini Afghanistan ambayo tegemeo kubwa la kipato ni kwa kuchunga kondoo na mbuzi lakini COVID-19 imepeperusha kipato chao, Mir Baaz Amir Ali Kherli ni miongoni mwa walioathiriwa akisema kuwa, “COVID-19 imetuathiri sana, hatuwezi kuuza maziwa, mtindi wala jibini. Maduka yote yamefungwa kwa hiyo hakuna pahala popote pa kuuza bidhaa zetu.”

Wakuchi walizoea kuuza bidhaa zao maeneo ya mbali lakini sasa wanauzia maeneo ya karibu na bei zinakuwa za chini ambapo Candra Samekto, Meneja wa IFAD Afghanistan anasema kuwa, “wakuchi tayari wanakabiliwa na changamoto kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mazingira yaliyomomonyoka. Sasa na mlipuko wa COVID-19 na kuzuiwa kuhamahama hawawezi kabisa kufikia masoko. Ina maana wanalazimika kuuza bidhaa zao, mifugo yao katika bei ya chini. Mfano, kwenye maeneo ya Nangarhar na Logar, wanauza mifugo yao kwa bei ya chini ya asilimia 40 ya bei waliyouza kabla ya janga la Corona.”

Hali inakuwa ngumu zaidi kuelewa kuhusu Corona kwa sababu wengi wao hawajui kusoma na kuandika ambapo Ali Khel anasema kuwa, “tutapata wapi taarifa kuhusu COVID-19. Hatuna televisheni, hatuna hata umeme, sasa tunawezaje kutazama televisheni.”
Hata hivyo mwezi Machi Corona ilipoibuka, IFAD kupitia mradi wa pamoja na serikali ya Afghanistan, wa mifugo na kilimo kwa jamii, CLAP, ilipatia mafunzo wafanyakazi wa kilimo wa ughani jinsi ya kujilinda dhidi ya Corona.
Walitumia picha badala ya maneno na walisambaza vikasha vya kujisafi ikiwemo barakoa na sabuni kwa familia 48,000 za wakuchi.

Bwana Ali Kheli anasema kuwa msaada huo angalau sasa wanaweza kujikinga dhidi ya virusi.

Mwezi Aprili pia IFAD ilizindua mradi wa kujikwamua kwa familia maskini za vijijini kwa kuanzisha mfuko wa kuwezesha jamii za vijijini kuendelea kulima na kuuza mazao yao hasa kupata pembejeo, taarifa, kufikia masoko na kuhakikisha wana kipato.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter