Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 inakumbusha jukumu la mabunge katika kuimarisha jamii- Guterres 

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (katika picha hii ya maktaba) alipohutubia kikao maalum cha Bunge la Italia
UN /Rein Skullerud
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (katika picha hii ya maktaba) alipohutubia kikao maalum cha Bunge la Italia

COVID-19 inakumbusha jukumu la mabunge katika kuimarisha jamii- Guterres 

Afya

Leo ni siku ya mabunge duniani ambapo Umoja wa Mataifa unasema ni siku muhimu ya kutambua mchango muhimu wa mabunge katika kupaza sauti za wananchi na pia kushawishi uundaji wa sera.

Katika ujumbe wake hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema kuwa “mimi nimewahi kuwa mbunge, na ninaguswa sana na wajibu na heshima ya kuwakilisha wananchi na kukidhi matarajio yao. Mabunge yana jukumu mahsusi katika kusongesha haki za binadamu na kusongesha maendeleo endelevu.”

Katibu Mkuu amesema kuwa kuliko wakati wowote ule, hivi sasa katika zama za janga la la virusi vya Corona au COVID-19, jamii inakumbushwa majukumu hayo muhimu.

 “Kadri dunia inapokabiliana na janga hili, tunaona umuhimu wa kipekee wa uwepo wa mifumo thabiti ya afya, mitandao ya uhakika na bora ya hifadhi ya jamii na ukuaji uchumi wa kutosheleza unaochechemua ajira zenye hadhi,” amesema Katibu Mkuu.

Bwana Guterres ameenda mbali zaidi akisema kuwa, “tunaona pia wale walio hatarini zaidi kwenye jamii zetu kama vile wanawake wakibeba mzigo mkubwa. Ukosefu wa usawa, unyanyapaa, mgawanyiko na utete katika dunia yetu vimeongezeka maradufu mbele ya macho yetu.”

Amesema kwa kuzingatia mazingira ya sasa, “ni lazima tuchukue hatua pamoja kujenga upya, mustakabali wenye usawa zaidi, wenye mnepo na wenye manufaa kwa wote. Nasihi mabunge ya nchi kokote pale kutekeleza kwa kina majukumu yao na kusongesha hatua endelevu na jumuishi.”

Katibu Mkuu amesema hilo linapaswa kujumuisha na kuratibiwa pamoja na mashirika ya kiraia, ili kuwa na mipango ya kitaifa dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Amesema na wakati huo, “tukumbuke kuwa hakuna taifa ambalo linaweza kufanikiwa peke yake. Hebu na tutumie fursa hii kujenga upya mustakabali wetu wa pamoja, tuchukue hatua za kijasiri na kubwa kwa tabianchi na kuweka haki za binadamu  na utu kuwa kitovu cha kazi yetu.”

Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania akiongoza Bunge wakati wa moja ya vikao vya mkutano wa Bunge la 11 lililomaliza muda wake hivi karibuni.
Tanzania Parliament Video
Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania akiongoza Bunge wakati wa moja ya vikao vya mkutano wa Bunge la 11 lililomaliza muda wake hivi karibuni.

SPIKA WA BUNGE LA TANZANIA JOB NDUGAI AZUNGUMZA

Miongoni mwa mabunge yaliyoendelea na vikao katikati ya janga la  COVID-19 ni Bunge la Tanzania ambapo wake, Spika Job Ndugai anasema, "tulipata changamoto nyingi ambazo zilisababisha pawe na mabadiliko makubwa ya utendaji kazi ndani ya ukumbi wa bunge na katika mazingira ya kibunge. Ambapo utaratibu wa bunge mtandao ndio ulisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika uendeshaji wetu wa bunge lakini tulichukua hatua nyingi kuweka maeneo mengi ya kuweza kunawa mikono kwa maji tiririka sabuni, kutumia dawa maalum, barakoa na tukaanza kutumia kumbi kadhaa wala sio ukumbi mmoja, ambazo zikawa zinaunganishwa kwa utaratibu wa mikutano ya video"

HOFU ILIKUWA CHANGAMOTO KUBWA KWA WABUNGE, WATUMISHI WA BUNGE NA WANANCHI

Na jambo gani basi walilopambana nalo zaidi? Spika Ndugai anasema, "kikubwa ambacho tulipambana nacho ni hofu ambayo waheshimiwa wabunge pamoja na watumishi wa bunge  na wananchi kwa ujumla walikuwa wamepata taarifa za ugonjwa huu ambazo hazikuwa zinaeleweka vizuri na watu walio wengi. Tunamshukuru Mungu pamoja na  hofu hiyo kubwa tuliweza kufanya kazi mwanzo mwisho ambapo tulimaliza shughuli zetu tarehe 16  mwezi wa Juni mwaka 2020. Hakika ugonjwa huu umetingisha sana bunge letu na  umesababisha mabadiliko ambayo yatakaa kwa muda mrefu sana miongoni mwetu na huenda yakawa ni mabadiliko ya moja kwa moja katika namna ya utendaji kazi wetu.Mabadiliko ambayo yaliyo mengi yametusababisha kufanya kazi katika njia za mtandao zaidi kuliko njia ambazo tumekuwa tukizitumia hapo mwanzo."

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio lake namba A/72/278  la tarehe 22 mwezi Mei mwaka 2018, lilipitisha Juni 30 kuwa siku ya mabunge duniani kwa kutambua mchango wa chombo hicho katika mipango na mikakati ya kitaifa katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Tarehe hiyo ya Juni 30 ni tarehe ambapo pia mwaka 1889, chama cha mabunge duniani, IPU kilianzishwa.