Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yachunguza video inayoonesha watu wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wake wakiwa kwenye "tendo la ngono" ndani ya gari

Makao makuu ya UNTSO mjini Yerusalem
UN /John Isaac
Makao makuu ya UNTSO mjini Yerusalem

UN yachunguza video inayoonesha watu wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wake wakiwa kwenye "tendo la ngono" ndani ya gari

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi wa video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii wikii hii ikionesha gari lenye nembo ya Umoja wa Mataifa likiwa kwenye mitaa yenye pilikapilika huku mwanamke mmoja akiwa amemkalia mwanume mmoja kwenye kiti cha nyuma cha abiria wakionekana wakifanya ngono huku watu wengine wakiwa kwenye gari hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric,  ametoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini New York Marekani leo Ijumaa mchana, akithibitisha kuwa video hiyo yenye urefu usiozidi nusu dakika, ina wafanyakazi ambao “ yawezekana ni watumishi wanaofanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia utekelezaji wa mkataba wa kusitisa mapigano”, au UNTSO.

Kwa mujibu wa taarifa, video hiyo, ilipigwa nyakati za usiku kwenye mtaa wa HaYarkon, mtaa wenye pilikapilika mjini Tel Aviv, lakini hadi sasa chanzo chake hakifahamiki na uhalali wake haujathibitishwa.

UNTSO ni nini?

Ujumbe huo ulikuwa ni ujumbe wa kwanza kabisa wa ulinzi wa amani ulioanzishwa mwaka 1948, ukijumuisha waangalizi wa kijeshi wa kusimamia mikataba ya kusitisha mapigano na kuzuia mizozano ya kijeshi ambapo makao makuu yake ni Yerusalem.

Tumeshtushwa sana na kuvurugwa na kile kinachoonekana kwenye video hiyo- Stéphane Dujarric, Msemaji wa UN

Kwa sasa UNTSO una waangalizi wa kijeshi 153, watumishi wa kimataifa 91 na kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, ina wanajeshi kutoka zaidi ya nchi 20.
Waangalizi wa kijeshi wanapelekwa katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwenye mpaka wa Israel na Lebanon na pia kwenye milima ya Golan.

Tabia hii ni kinyume na kila kitu ambacho tunakisimamia

“Tumeshtushwa sana na kuvurugwa na kile kinachoonekana kwenye video hiyo,” amesema Bwana Dujarric akiongeza kuwa, “tabia kama hiyo inachukiza na ni kinyume na kila kitu ambacho tunakisimamia na hasa tunapokuwa tunahaha kufanikisha maadili mema miongoni mwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.”

Amewaambia waandishi wa habari wakati wa mkutano wake nao kwa njia ya video kuwa, “tumefahamu kuhusu video hiyo takribani siku mbili zilizopita na wenzetu kwenye ofisi ya uchunguzi, OIOS walianza kazi haraka. Uchunguzi wao naamini unakwenda haraka. Tunafahamu eneo la tukio, lakini utambulisho wa wahusika kwenye video hiyo ambao wanaweza kuwa ni wafanyakazi wa UNTSO karibu unakamilika.”

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uchunguzi wa OIOS unatarajiwa kukamilika haraka sana na hatua sahihi zitachukluiwa haraka.

UNTSO kauli yake ni ipi?

 UNTSO nayo imetoa taarifa ikiongeza kuwa inasimamia msingi wa Umoja wa Mataifa wa kutovumilia kituo chochote cha ukosefu wa maadili kama hicho, ikiwemo ukatili wa kingono, unyanyasaji na imekumbusha wafanyakazi wake juu ya wajibu wao kwenye kanuni ya maadili ya Umoja wa Mataifa.

“Kama ilivyo azma ya Umoja wa Mataifa kuhusu uwazi, chombo hiki kitawapatia taarifa kuhusu matokeo ya uchunguzi na hatua zitakazochukuliwa,” amesema Bwana Dujarric.