Skip to main content

UNMISS yashirikiana na Kanisa Katoliki kusambaza barakoa katika masoko ya Yambio Sudan Kusini

Wakazi wa Yambio wakiendelea na shughuli zao kwenye eneo la soko
UN /Nektarios Markogiannis
Wakazi wa Yambio wakiendelea na shughuli zao kwenye eneo la soko

UNMISS yashirikiana na Kanisa Katoliki kusambaza barakoa katika masoko ya Yambio Sudan Kusini

Afya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, ili kusaidia kuwakinga watu dhidi ya COVID-19, umeunganisha nguvu na Kanisa Katoliki jimbo la Yambio-Tambura kusambaza barakoa zilizotengengenezwa kienyeji kwa jamii za maeneo hayo.

Soko hili mjini Yambio shughuli za kuuza na kununua bidhaa zinaendelea. Watu wa hapa wanafahamu kuhusu hatari ya uwepo wa ugonjwa wa COVID-19 na uhitaji wa kuweka umbali kati ya mtu na mtu ili kuepuka kusambaza virusi vya corona, lakini wanahisi hawana namna isipokuwa kuendelea na maisha yao ya kawaida kwasababu bila kufanya kazi leo, inamaanisha kutopata mlo wa familia zao ifikapo kesho.

Ili kusaidia angalau kuweka kinga fulani, UNMISS imefanya kampeni inayowalenga watu walioko hatarini zaidi katika masoko ya pembezoni katika mji wa Yambio. Wauzaji katika masoko hayo wanashukuru kwani wanatambua kuwa wako hatarini. Awadia Mahmud ni mmoja wao, anasema,“wametusaidia kwa kutuletea barakoa ambazo tunaziweka kwenye pua na midomo yetu kujikinga. Kama virusi hivi vinakuja kupitia hewa, tunapofunika pua zetu, vitaishia katika barakoa. Tunapofika nyumbani usiku, tunaifua na kuiacha ikauke kisha tunaivaa asubuhi. Hii itatulinda sana. Kipindi cha nyuma tulipokea pipa ambalo tunalijaza maji na tunayatumia kunawa mikono kila asubuhi tunapokuja sokoni.”

Familia ya Umoja wa Mataifa inafanya kazi kwa bidii kusaidia mkakati wa serikali kuilinda jamii, mkakati unaoongozwa na kikosi kazi cha ngazi ya juu dhidi ya COVID-19 cha Equatoria Magharibi. Emmanuel Dukundane ni Afisa wa UNMISS anayeshughulikia masuala ya kiraia huko Yambio, anasema,“tunalenga barakoa 500 kwa kila eneo na tuna maeneo manne katika Equatoria Magharibi.Hivi sasa tuko hapa katika soko la Posu, ambalo liko katika moja ya viunga vya mji wa Yambio ambako tunasambaa barakoa hizi tukizilenga jamii katika soko ambako wengi ni wanawake. Hizi ni kusaidia tu watu au jumuiya ya wanawake hapa katika soko ambao wako hatarini kuambukizwa virusi vya corona. Hii ni moja ya njia za kuzuia COVID-19 hapa Yambio. Barakoa nyingi zimesambazwa lakini ni mchakato endelevu. Tunayalenga maeneo haya kuhakikisha kuwa kila mtu ana njia za kujikinga kupitia barakoa ambazo zinaweza kwa pamoja kuhamasisha juhudi za kikosi kazi cha ngazi ya juu cha Equatoria Magharibi.”

Ugawaji wa Barako ni moja ya mipango mingi inayofanywa na UNMISS katika eneo la Equatoria Magharibi ili kushughulikia janga la COVID-19. Ujumbe huo wa kulinda amani pia umefanya kampeni ya kuelimisha umma katika miji na vijiji kote katika eneo hilo ili kuongeza uelewa kuhusu hatari zilizopo na kuzisaidia jamii ili ziweze kujiweka salama na kuwaweka  wengine salama.