Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhusiano baina ya wababe Marekani, China na Urusi haujawahi kuwa mbaya kuliko sasa:Guterres

Vijana wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa huko Lusaka wanashiriki katika kuelimisha jamii juu ya virusi vya corona.
UNDP Zambia
Vijana wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa huko Lusaka wanashiriki katika kuelimisha jamii juu ya virusi vya corona.

Uhusiano baina ya wababe Marekani, China na Urusi haujawahi kuwa mbaya kuliko sasa:Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika dunia ambayo imeghubikwa na misukosuko na majanga kama virusi vya Corona au COVID-19, mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi , ongezeko la pengo la usawa na watu kutotendewa haki kwa misingi ya rangi , changamoto yetu ya pamoja kama jumuiya ya kimataifa ni kuyakabilia haya amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Antonio Guterres ameyasema hayo leo wakati wa mkutano wa waandishi wa Habari kabla ya maadhimisho ya miaka 75 ya kupitishwa kwa katiba ya Umoja wa Mataifa ambayo ilipitishwa 26 Juni 1945.

Amesisitiza kwamba wakati majanga haya yakiikabili dunia viongozi wa dunia lazima wawe wanyenyekevu na kutambua umuhimu mkubwa wa mshikamano na umoja hususan katika wakati wa COVID-19, mabadiliko ya tabianchi, kuhodhi masuala ya anga na hatari ya uzalishaji wa nyuklia.

Ameongeza kuwa “Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kutabiri nini kitakachofuata, tuko katikati ya ukungu na kila tuwezapo Umoja wa Mataifa umepenyeza katika ukungu huo na kuchukua hatua. Familia ya Umoja wa Mataifa imejikusanya ili kuokoa maisha, kudhibiti maambukizi ya virusi na kupunguza athari za kiuchumi.”

Guterres amesisitiza kwamba hatuwezi kumudu kurejea katika hali ya zamani na kujenga mfumo ambao utachochea mgogoro “Lazima tujijenge vyema kwa kuwa na jamii na uchumi endelevu, jumuishi nawenye usawa wa kijinsia. Hakuna sababu kwa mfano kwa nchi yeyote kujumuisha makaa ya mawe katika mikakati yake ya kujikwamua na COVID-19”. Huu ni wakati wa kuwekeza katika rasilimali za nishati ambayo haichafui mazingira , yenye kuunda ajira zenye hadhi na kuokoa fedha. Umoja wa Mataifa umedhamiria kuongoza katika nishati endelevu.”

Katibu Mkuu pia alitumia nafasi hiyo kuwasilisha uzinduzi wa ripoti ya muongozo wa hatua za Umoja wa Mataifa za kukabiliana na COVID-19 ambao sio tu umeorodhesha hatua zilizochukuliwa na Umoja huo katika miezi mitatu iliyopita lakini pia unatoa mtazamo wa kuelekrea kujikwamua vyema.

Mafanikio ya UN wakati wa COVID-19

Miongoni mwa mafanikio ya Umoja wa Mataifa aliyoaorodhesha wakati wa janga la COVID-19 ni Pamoja na

  • Kusafirisha Zaidi ya vifaa milioni 250 vya kujikinga kwa Zaidi ya nchi 130
  • Kuhakikisha elimu kwa Watoto milioni 155
  • Kutoa msaada wa afya ya akili kwa Watoto milioni 45, wazazi na watoa huduma
  • Kuuweka mnyororo wa mtandao wa usambazaji wa Umoja wa Mataifa katika huduma kwa nchi wanachama na kuanzisha vituo vinane vya kimataifa vya usafiri wa anga ambavyo vimeweza kuzifikia nchi 110 na kutoa vifaa tiba vya ukubwa wa mita 69,000 katika wiki sita zilizopita pekee.
  • Kutoa mafunzo kwa watu milioni 2 wahudumu wa kijamii na wahudumu wa afya
  • Kuanzisha mifumo salama kwa Watoto milioni 3 na watu wazima ili kutoa taarifa za visa vya unyanyasaji na ukatili wa kingono.
  • Kupata taarifa za jinsi gani ya kubaki salama na fursa za huduma za afya kuwafikia watu zaidi ya bilioni 2.

Miaka 75 ya utoaji huduma

Kuhusu utendaji wa shirika wakati wa miaka hii 75 tangu kupitisha kwa katiba ya Umoja wa Mataifa, Guterres ameonyesha kwamba “Tumejaribu kusaidia kuunganisha ulimwengu kuwa na ushirika mzuri kwa ajili ya kutatua changamoto za dunia na kwa ajili ya faida ya wote.”

Na kisha akaorodhesha kazi za kila siku za Umoja wa Mataifa duniani kote na kueleza kwamba amesikiliza majibu ya utafiti wa UN75 ambapo watu zaidi ya 230,000 kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa walishiriki.

Utafiti huo ulijikita katika vipaumbele vitatu vya msingi: huduma za afya kwa wote, kuimarisha mshikamano baina ya watu na mataifa na kuufikiria upya uchumi dhidi ya usawa.

Miaka 75 ya katiba ya UN

Katibu Mkuu amesema “wakati tukisherehekea siku ya katiba ya UN na kuganga yajayo ni lazima tufikirie upya jinsi gani mataifa yanashirikiana.”

Amesema miongoni mwa mahitaji muhimu ni haja ya kuwa na ushirikiano wa kimataifa ambao unahusiana , kuyaleta Pamoja mashirika ya kikanda ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, taasisi za kimataifa za fedha na mashirika mengine, ujumuishi, mchango mkubwa wa asasi za kijamii , makampuni ya biashara, miji, dini na vijana, na utendaji ambao unafanyakazi kama nyenzo ya mwongozo wa kimataifa mahali popote utakapohitajika.

Ameongeza kuwa “Tatozo sio kwamba ushirikiano wa kimataifa hauko tayari kwa changamoto zinazoikabili dunia. Tatizo ni kwamba ushirikiano wa sasa unapungukiwa na kiwango, matamanio na nguvu.”

Mmoja wa watu wakujitolea huko Lusaka akimuongelesha/kumuelimisha mwanamke huyu kuhusu C0VID-19
UNDP Zambia
Mmoja wa watu wakujitolea huko Lusaka akimuongelesha/kumuelimisha mwanamke huyu kuhusu C0VID-19

 

Amekiri kwamba kuna ugumu wa kufikia mabadiliko yenye maana ya mfumo wa utawala wa dunia “bila ushiriki wa mataifa yenye nguvu duniani na ngoja nianike wazi kwamba uhusiano leo hii haujawahi kuwa mbovu kuliko wakati mwingine wowote.”

Na baadaye alipoulizwa swali kuhusu nani ndio wababe hao katika kubomoa ushirikiano Guterres akaweka bayana kwamba wawili ni mataifa makubwa yenye nyuklia  na uchumi mkubwa Urisi na Marekani wakishika nafasi ya kwanza na taifa hilo la Amerika Kaskazini na Uchina katika nafasi ya pili.

Hivyo akasema “Kaka kuna husiano ambazo ziko vibaya hivi sasa na hazifanyi kazi bila shaka ni hizo na tunaona wazi athari zake katika wakati ambao tunahitaji kuchagiza ulimwengu wote kulishinda janga la COVID-19, kuyashinda mabadiliko ya tabianchi, kurejesha utulivu angani na kuhakikisha uzalishaji wa nyuklia hatuo tishio jipya ambalo linaweza kuwepukika.”

Hata hivyo alikuwa na matumaini kwamba kutakuwa na “Mwamko mpya wakati tutatambua udhaifu wetu wa Pamoja na mwamko huu utafanyika wakati sababu zinazotugawanya hii leo , badala yake kuwalazimisha watu kuelewa kwamba mgawanyiko ni hatari kwa kila mtu kuanzia kwao wenyewe. Na hatimaye huo ndio mlango wa kutoka kwenye ukungu unaotughubika na katika yetu bado inatuonyesha mlango huo.”