Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC umetokomezwa, WHO yapongeza

Wauguzi wakisherekea  mwisho wa janga la Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo wafanyakazi zaidi ya 200 walifanya kazi bila kuchoka kulinda watoto kutokana na ugonjwa huo.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Wauguzi wakisherekea mwisho wa janga la Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo wafanyakazi zaidi ya 200 walifanya kazi bila kuchoka kulinda watoto kutokana na ugonjwa huo.

Mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC umetokomezwa, WHO yapongeza

Afya

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imetangaza kutokomezwa kwa mlipuko wa 10 wa Ebola  mashariki mwa nchi hiyo ulioanza mwezi Agosti mwaka 2018. 

Tangazo limetolewa hii leo kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa na Waziri wa Afya wa nchi hiyo,  Dkt. Eteni Longondo, hatua ambayo imepongezwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus.

Akizungumzia hatua hiyo, Dkt. Tedros amesema“leo ni siku ya furaha, nafurahia kusherehekea kutokomezwa kwa Ebola nchini DRC ambako zaidi ya watu 1,100 waliougua Ebola na kupona, walirejea na afya njema kwa familia zao na huu ni ushuhuda wa huduma za tiba zilizotolewa na wafanyakazi wa afya nchini humo, wakiungwa mkono na WHO na wadau wengine.”

Ameongeza kuwa, “kutokomezwa kwa Ebola ni ushindi wa sayansi. Kasi kubwa ya kupelekwa  chanjo yenye ufanisi mkubwa  kuliokoa maisha na kulipunguza kasi ya maambukizi na kwa mara ya kwanza sasa dunia ina chanjo iliyothibitishwa dhidi ya Ebola. Tiba fanisi nazo zilibainishwa ambazo zilipunguza kwa kiasi kikubwa tishio pindi mgonjwa alipotibiwa haraka. “

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO ametuma pongezi za kipekee kwa madaktari, wahudumu wa afya na wafuatiliaji waliokwenda nyumba kwa nyumba kusaka wagonjwa wapya huku akikumbuka wahudumu wa afya waliopoteza maisha akisema WHO itaendelea kusisitiza umuhimu wa usalama wao.

WHO imepongeza pia nchi 9 jirani na DRC ambazo imesema zilikuwa na mchango mkubwa katika kutokomezwa kwa Ebola Mashariki mwa DRC.

Hata hivyo WHO imesisitiza kuwa hakuna kubweteka kwa kuwa kuna mlipuko mwingine wa Ebola huko Mbandaka jimboni Equateur na kusema kuwa hata zilizochukuliwa mashariki mwa DRC kutokomeza Ebola zitumike pia Mbandaka na dhidi ya Surua na ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Jumla ya watu 2,200 walifariki dunia kutokana na mlipuko huo wa 10 wa Ebola huko mashariki mwa DRC ulioanza Agosti 2018.