Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde Israel acheni upanuzi wa makazi ya Walowezi Ukingo wa Magharibi:UN

 Makaazi  ya Beit Hadassah katika eneo la H2 huko Hebroni, West Bank
UNRWA/Marwan Baghdadi
Makaazi ya Beit Hadassah katika eneo la H2 huko Hebroni, West Bank

Chonde chonde Israel acheni upanuzi wa makazi ya Walowezi Ukingo wa Magharibi:UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwa njia ya video kwenye Baraza la Usalama hii leo ametoa wito kwa Israel na kuisihi kutotekeleza mipango yake ya upanuzi wa makazi ya walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi.

Katika kikao hicho kilichomulika hali ya Mashariki ya Kati na mchakato wa amani ya eneo hilo Guterres amesema “Natoa wito kwa serikali ya Israel kuachana na mipango ya ujezi wa makazi ya walowezi, endapo mipango hiyo itatekelezwa basi itakuwa inafanya ukiukwaji mkubwa wa sharia za kimataifa , na kuathiri sana matarajio ya suluhu ya kuwa na mataifa mawili na pia kuhatarisha uwezekano wa kuanza tena kwa majadiliano.”

Makazi ya walowezi yanakiuka sheria za kimataifa

Mbele ya wajumbe wote 15 wa Baraza la Usalama Katibu Mkuu amesema tumefikia wakati wa kufanya maamuzi akisistiza kwamba “Tishio la Israel la upanuzi wa makazi hayo kwenye eneo linalokaliwa la Wapalestina Ukingo wa Magharibi linatia wasiwasi kwa wapalestina, Waisrael wengi na jumuiya ya kimataifa.

Antonio Guterres ameainisha pia kuhusu ongezeko la kutetereka kwa uchumi kutokana na janga la COVID-19, kupunguzwa kwa msaada wa wahisani na maamuzi ya hivi karibuni ya Palestina kutokubali tena mapato ya mpakani ambayo Israel hukusanya kwa niaba ya mamlaka ya Palestina, amesema sababu zote hizi kwa mtazamo wake zinaongeza hatari ya madhila kwa wapalestina.

Guterres amerejelea kusisitiza kwamba ataendelea kuzisaidia pande zote Palestina na Israel kutatua mzozo na kumaliza ukaliwaji kwa mujibu wa sharia za kimataifa, maazimio ya Umoja wa Mataifa na makubaliano yaliyoafikiwa ili kufikia malengo ya kuwa na mataifa mawili Israel na Palestina iliyo huru ambayo yataweza kuishi Pamoja kwa amani na usalama kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa.”nawachagiza wahisani wa kikanda na kimataifa wanaounga mkono suluhu ya mataifa mawili kusaidia kuzirejesha pande hizi kwenye njia ya majadiliano na suluhu ya amani.”

Na kwa upande wa viongozi amewapa wito akisisitiza “Viongozi lazima wachukue hatua kwa makini, utaratibu na kuonyesha kuna utashi wa kusongesha mbele lengo la haki na amani ya kudumu.”

Mipango ya Israel

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliifanya mipango hiyo ya upanuzi wa makazi ya Walowezi kama ahadi wakati wa kampeni za kabla ya uchaguzi wa kitaifa uliofanyika mwezi Machi.

Na mipango hiyo itashuhudiwa uhuru wa mipaka ya Israel ukiongezwa kwa asilimia 30 kwenye Ukingo wa Magharibi  na kuchukua sehemu kubwa ya bonde la Jordan na mamia ya makazi haramu ya Israel.

Ili kukabiliana na mipango hiyo viongozi wa Palestina wamekata uhusiano wowote na Israel na Marekani nchi ambayo inaunga mkono mipango hiyo ya Israel.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nikolay Mladenov ameonya Baraza la Usalama kwamba miongo mitatu ya juhudi za kimataifa za amani inaweza kuwa njiapanda.

“Kutambua kwamba watu wote wana haki ya kuishi katika nyumba zao, miaka 27 iliyopita viongozi wa Israel na Palestina waliafiki kuanza safari ngumu, kutatua mgogoro huo kupitia majadiliano bila kuchukua hatua binafsi ili kufikia kilele cha muafaka wa amani , lakini leo hii tuko mbali na lengo hilo kuliko wakati mwingine wowote.”

Hofu ya machafuko

Bwana. Mladenov amearifu kwamba malaka ya Palestina hivi sasa imeacha kupokea kodi inayokusanywa na Israel kwa niaba yake ma matokeo yake yamesababisha kushuka kwa asilimia 80 kwa mapato ya kila mwezi na kuongeza athari katika uchumi ambao unayumba kutokana na COVID-19, na kupunguzwa kwa msaada kwa shirika la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

Ameongeza kuwa Wapalestina wanaoishi kwenye Ukanda wa Gaza chini ya udhibiti wa Hamas kufuatia mvutano wa zaidi ya muongo mmoja wako katika hatari zaidi amesema Mladenov na kuongeza kuwa “Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yameombwa kutaribu hatua za Pamoja na kubeba jukumu, wakati tukijiandaa kutoa msaada kwa misingi ya dharura , Umoja wa Mataifa hauwezi kuwa mbadala wa mamlaka ya Palestina, hivyo ni muhimu sana kwa wahudumu wa misaada ya kibinadamu na misaada mingine kutocheleweshwa au kuzuiliwa.”