Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vinavyotokana na VVU, TB na Malaria vinaweza kuongezeka maradufu katika miezi 12 ijayo-Ripoti

Mtoto akipokea dawa za TB nchini Sudan Kusini kwa msaada wa Global Fund kupambana na VVU,TB na Malaria
UNDP South Sudan/Brian Sokol
Mtoto akipokea dawa za TB nchini Sudan Kusini kwa msaada wa Global Fund kupambana na VVU,TB na Malaria

Vifo vinavyotokana na VVU, TB na Malaria vinaweza kuongezeka maradufu katika miezi 12 ijayo-Ripoti

Afya

Ripoti mpya ya  fuko la kimataifa la ufadhili Global Fund iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi inakadiria kuwa nchi ambazo zimeathirika na Virusi Vya UKIMWI, VVU, Kifua Kikuu yaani TB na Malaria, kwa haraka zinahitaji dola bilioni 28.5 za kimarekani ili kulinda hatua kubwa zilizokwisha kufikiwa katika miongo miwili iliyopita katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo matatu.

Ripoti hiyo inayoangazia madhara ya ugonjwa wa COVID-19 kwa nchi hizo imesema magonjwa hayo matatu bado yanawaua zaidi ya watu milioni 2.4 kila mwaka. Tangu mwaka 2002, ushirikiano wa Global Fund umesaidia kuokoa zaidi ya maisha ya watu milioni 32 na kukata idadi ya vifo vinavyotokana na VVU, TB na Malaria kwa nusu tangu majnga yalipokuwa katika kilele chake. Janga la COVID-19 hivi sasa linatishia kurejesha nyuma mafanikio hayo, imeeleza ripoti hiyo.

Mbali ya vifo vya moja kwa moja vya COVID-19 ambavyo vinaweza kuwa janga katika nchi zilizoko hatarini zaidi, makadirio yanaeleza kuwa vifo vinavyotokana na VVU, TB na Malaria vinaweza kuongezeka maradufu ikiwa mifumo ya afya itaelemewa, programu za matibabu na kukinga zitavurugwa na pia rasilimali kuelekezwa kwingine.

“Kidunia, hii inamaanisha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na VVU, TB na Malaria, kwa mwaka vinaweza kurejea tena katika viwango ambavyo havijaonekana tangu kipindi ambacho magonjwa hayo yalikuwa yanaua zaidi na hivyo kuteketeza mafanikio yote yaliyofikiwa takribani  miongo miwili iliyopita.” Ripoti hiyo ya Global Fund imefafanua.

Global Fund inasema kuongeza kwa ushughulikiaji madhubuti dhidi ya COVID-19 na kupunguza athari za VVU, Kifua Kikuu na Malaria itahitaji rasilimali nyingi zaidi kuliko ambazo zimepatikana hadi kufikia  sasa. Fuko hilo la dunia limefanya kazi na wadau kukadiria mahitaji yanayowezekana kuwa yanahitajika  katika nchi ambazo Global Fund inafadhili.

“Tunakadiria kuwa takriban dola bilioni 28.5 za kimarekani zinahitajika kwa miezi 12 ijayo kurekebisha programu za VVU, Kifua Kikuu na ugonjwa wa Malaria ili kupunguza athari za COVID-19, kutoa mafunzo na kulinda wafanyakazi wa afya, kuimarisha mifumo kwa afya ili isianguke, na kuikabili COVID-19 yenyewe, hasa kupitia upimaji, kutafuta na kutengwa na kwa kutoa matibabu. Hii haijumuishi gharama za chanjo.”  Imeeleza ripoti.