Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante wadau wa kimataifa msaada wenu unapambana na corona Somalia:Swan 

Mwanamke akipita pembeni ya gari la wagonjwa ndani ya hospitali ya Benadir mjini Mogadishu, Somalia.
UN /Ilyas Ahmed
Mwanamke akipita pembeni ya gari la wagonjwa ndani ya hospitali ya Benadir mjini Mogadishu, Somalia.

Asante wadau wa kimataifa msaada wenu unapambana na corona Somalia:Swan 

Afya

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa mpango wa Umoja huo nchini Somalia UNSOM, James Swan amesema msaada uliotolewa na wadau wa kimataifa umeisadia Somalia kuweka kituo kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa corona au COVID-19, na kuwataka wadau hao kuongeza msaada zaidi kwa serikali. 

Mjini Moghadishu, hospitali ya De Martin, ni kituo muhimu kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19 nchini humo  mkuu wa UNSOM James Swan anazuru kujionea hali halisi ya huduma na kuzungumza na wahudumu wa afya walio msitari wa mbele kupambana na janga hili la corona.

Swan amesema mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yanaisaidia Somalia kupambana na COVID-19 kupitia shirika la afya duniani WHO, la kuhudumia watoto UNICEF, la uhamiaji IOM na mashirika mengine mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yamechangia.

Na baada ya kuzunguka hospitali nzima Bwana Swan akaketi na wahudumu wa afya wa hospitali hiyo na kuwashukuru

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan akihutubia Baraza la Usalama.
UN Photo/Manuel Elías
Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan akihutubia Baraza la Usalama.

“Napenda kutoa shukran zangu za dhati kwa wahudumu wa afya mlio msitari wa mbele, wahudumu wa dharura ambao wako katika nafasi ya kusaidia ambao wanatoa huduma muhimu, matibabu, wamesaidia katika upimaji na kutoa huduma nyingine na bila shaka kuwatibu wagonjwa wa corona. Mko msitari wa mbele nyie ndio mnaotoa huduma kwa walioathirika na ugonjwa huu, na mnashukuriwa naamini na taifa lenu lakini pia na marafiki na washirika wenu.”

Msaada wa Umoja wa Mataifa wa COVID-19 kwa Somalia unajumuisha , mipango, uratibu, uandaaji wa sera za msaada, kuijengea uwezo wa wataalam wa afya nchi hiyo ambao wanaofanyakazi katika maabara na hospitali na kusimamia maabara za upimaji mjini Moghadishu, Garowe na Hargeisa. Pia wanatoa vifaa vya kujikinga na corona na msaada wa kuendesha hospitali, maabara na vituo vya kutenga wagonjwa .

Naye waziri wa afya na huduma za jamii wa Somalia Bi. Fawziya Abikar Nur ameyashukuru mashirika ya umoja wa Mataifa na wadau wengine kwa msaada waliotoka ingawa akisemaNdio changamoto ni kubwa kama kawaida ya sekta ya afya lakini WHO inasaidia kwa upande wa wagonjwa na kudhibiti maambukizi katika vituo vyote, inatoa mishahara kwa wahudumu wetu wapya walioajiriwa na kuimarisha uchagizaji na ushirikishwaji katika jamii hususan kwenye maeneo ya kubaini na kufuatilia wagonjwa.”

Mwakilishi wa WHO nchini humo amesema hatua kubwa imepigwa na wagonjwa wapya wameanza kupungua lakini sio wakati wa kubweteka ni wakati wa kuwa makini zaidi.

Kwa mujibu wa WHO hadi Juni 20 Somalia ilikuwa na wagonjwa zaidi ya 2,755 waliothibitishwa kuwa na COVID-19, na vifo 88. Miongoni mwa wagonjwa 133 ni wahudumu wa afya.