Baada ya kurejea maisha ya kawaida wagonjwa wa COVID-19 waongezeka:WHO

22 Juni 2020

Shirika la afya duniani WHO leo limesema ugonjwa wa virusi vya corona au COVID-19 umeanza kushika kasi tena baada ya kuripotiwa visa vipya  zaidi ya 183, 000 kwa siku moja, ikiwa ni idadi kubwa zaidi hivi sasa.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya Habari iliyotolewa mjini Geneva UswisI na mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhamon Ghebreyesus takriban nusu ya visa hivyo vimeripotiwa katika nchi za Amerika, lakini Kusini mwa asia na Mashariki ya Kati nazo zinaripoti idadi kubwa ya wagonjwa.

Dunia iko katika duru mpya na ya hatari, watu wengi  inaeleweka kwamba wamechoka kukaa nyumbani, inaeleweka kwamba nchi zina hamasa ya kufungua jamii zao na uchumi, lakini virusi vinaendelea kusambaa kwa haraka, bado ni hatari kubwa na watu wengi wako hatarini kuvipata. Tunatoa wito kwa nchi zote na watu wote kujizuia na kuwa makini” ameongeza Dkt. Tedros.

Delphine Buysse
Wasanii wa Senegal wamechora michoro katika mji mkuu, Dakar, ili kuongeza uelewa juu ya COVID-19.

Kwa upande wake Dkt. Michael Ryan mkurugenzi mtendaji wa program ya dharura za kiafya wa WHO amesema “Hivyo mnaweza kuwa raundi ya pili ya kilele ya mlipuko ndani ya mlipuko wa kwanza kisha mnaweza kuwa na awamu ya pili ya mlipuko na sio hili au lile.”

Dkt. Ryan pia amesema huenda wimbi hili jipya la COVID-19 limeanzia Beijing na kusema “Nadhani haionyeshi kabisa kwamba chanzo chake ugonjwa huu ni Ulaya. Kinachoonekana ni kwamba wakati mmoj huenda ugonjwa huu ulikuja kutoka nje ya Beijing”.

Wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mnamo Juni 20 Filippo Grandi Kamishina mkuu wa wakimbizi akizungumza kwenye mkutano wa WHO na waandishi wa Habari alisisitiza kwamba “Wakimbizi, watu waliotawanywa na watu wengine walio safarini ni lazima wajumuishwe katika hatua za kitaifa za serikali za kukabiliana na janga hili. Ni dhahiri kwamba ukilitenga kundi hili itakuwa ni mtihani kwa wengine wote waliosalia.”

Hivi sasa hofu kubwa ya WHO ni kuhusu hatari iliyo bayana ya kusambaa kwa maambukizi ya COVID-19 kwenye makambi ya wakimbizi amesema Dkt. Tedros na kuongeza kuwa “ Zaidi ya hatari ya kiafya inayoletwa na virusi vya COVID-19, kingine ni kuwaweka wakimbizi wengi katika Maisha magumu zaidi.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud