Mr. Bean aunga mkono vita ya WHO dhidi ya COVID-19

22 Juni 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limeweka wazi hii leo kuwa kwa kushirikiana na makampuni mawili ya utengenezaji filamu wameungana na kuzindua tangazo kwa umma lililomshirikisha mchekeshaji nyota duniani Mr Bean kwa lengo la kuwaelimisha wanajamii kuhusu kujikinga na virusi vya Corona.

Makampuni Project Everyone na Tiger Aspect Production yametengeneza kikaragosi cha Mr Bean kikionesha orodha muhimu ya Mr Bean inayopaswa kufuatwa ili kujikinga na COVID-19.

Video fupi inamwonesha Mr Bean katika hali ya kikaragosi au ‘katuni’ akishusha bango lenye orodha ya mambo muhimu ya kuwalinda watu dhidi ya COVID-19. Maambukizi ya COVID-19 yakiendelea kushuhudiwa  kuongezeka duniani, “Orodha muhimu ya Mr Bean kuhusu COVID-19” ni ukumbusho kwa watu kuhusu umuhimu wa kunawa mikono na kutoshika uso, kukaa umbali kati ya mtu na mtu na kuonesha wema kwa majirani. Aidha bango limeshauri watu kufuatilia dalili na pia kuwasiliana na wataalamu wa afya ikiwa kuna uhitaji wa kufanya hivyo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, “COVID-19 inaathiri kila kitu katika maisha ya mwanadamu na tunahitaji kutumia kila zana na njia zozote zilizopo kusambaza taarifa za kuokoa maisha na watu wote duniani kote. Ninashukuru kwa msaada wa timu nyuma ya Mr Bean kwa kutumia sauti yenu na vipaji kusambaza ushauri muhimu kuhusu umbali kati ya mtu na mtu, kujisafi na kufahamu dalili.”

Sauti katika tangazo hilo la elimu kwa umma ni ya Rowan Atkinson ambaye jina lake la uigizaji ni Mr Bean. Muigizaji ambaye alimtengeneza Mr Bean kuwa ni ‘mtoto ambaye yuko katika umbo la mtu mzima’ alipokuwa katika  Chuo Kikuu cha Oxford akiwa na mtengeneza filamu na mchechemuzi wa Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs Bwana Richard Curtis.

Mr Bean ambayo ilianza kurushwa katika miaka ya 1990 kabla ya kubadilika na kuwa katika mfulululizo wa vikaragosi imeenea ulimwenguni ikiwa na wafuasi milioni 96 katika ukurasa wa Facebook na mashabiki kote India, Brazil na hata Indonesia. Mr Bean pia mwaka huu anaadhimisha miaka 30 ya uwepo wake.

Richard Curtis aliyeko nyuma ya Mr Bean anasema, “tunayo furaha kufanya kazi na WHO kuhusu kikaragosi cha Mr Bean na kuunga mkono ujumbe wa afya kuhusiana na COVID-19. Mnamo mwaka 2015 viongozi wa dunia waliweka ahadi katika malengo 17 kutokomeza umaskini, kutokomeza kutokuwepo kwa usawa na mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2030. Afya njema na ustawi ni lengo namba 3 na msingi wa kuyafikia malengo mengine. Ni muhimu kwamba tufanye kazi na wadau wabunifu na sekta zote zije pamoja kuendelea kutoa ujumbe nje kuhusu ni namna gani tunaweza kuidhibiti COVID-19 na kujenga upya dunia nzuri ambako malengo ya dunia yanasalia kuwa muongozo wa kufikiwa ifikapo 2030. Sina hakika ni sekta gani ambayo Mr Bean yumo lakini tunafurahi kuwa naye kwenye safari.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter