Siku ya Yoga, UN yaangazia mazoezi ya utamaduni wa zani kukabili COVID-19

Jon Witt, akifanya mazoezi ya Yoga Jersey City
Winnie Witt
Jon Witt, akifanya mazoezi ya Yoga Jersey City

Siku ya Yoga, UN yaangazia mazoezi ya utamaduni wa zani kukabili COVID-19

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya kimataifa ya Yoga ambayo ni maadhimisho ya sita ya Umoja wa Mataifa yanayofanyika kila mwaka Juni 21, kwa lengo la kutambua aina ya zamani ya mazoezi haya kama njia ya kuboresha afya na ustawi, lakini pia kama nyenzo yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto na msongo uliosababishwa na janga la virusi vya corona au COVID-19.

Yoga ni mfumo wa zamani wa mazoezi ya viungo, akili na nafsi ambao ulianzia India na sasa unafanyika katika muundo mbalimbali kote duniani. Neno Yoga linamaanisha jiunge au ungana, likiwa ni ishara ya muungano wa mwili na nafsi.

Kupambana na msongo na hofu

Wakati mlipuko wa janga la COVID-19 umepindua maisha ya watu kote duniani ongezeko la changamoto ikiwemo msongo wa mawazo na taharuki vinaonekana kana kwamba watu wanakabiliana na mabadiliko ya maisha.

Maadhimisho ya Yoga mwaka huu yameandaliwa na Ubalozi wa kudumu wa India kwenye Umoja wa Mataifa na kufanyika mtandaoni chini ya kaulimbiu “Yoga kwa ajili ya afya, Yoga nyumbani” kwa sababu ya kuchukua tahadhari ya kukabiliana na janga la corona ambalo limesababisha studio na vituo vingi vya yoga kufungwa na wataalam wa Yoga sasa wamegeukia kuendesha mazoezi hayo majumbani na mtandaoni.

Watu wakifanya mazoezi ya Yoga ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu kwenye makao Makuu ya UN , New York
Permanent Mission of India
Watu wakifanya mazoezi ya Yoga ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu kwenye makao Makuu ya UN , New York

Sike Von Brockhausen ambaye ni mfanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF mjini New York Marekani anayehusika na kuusaidia Umoja wa Mataifa kukabiliana na dharura za kimataifa anasema “Wakati wa kazi zangu na wakati huu wa kusalia majumbani , Yoga imenisaidia sana kuwa mtulivu, kuweka uwiano katika maisha yangu na kuwa na mtazamo.”

Yoga ni kitu cha tofauti

Wazazi wanaweza kuiona Yoga kama kitu cha kusaidia kuwafanya watoto wao wawe waulivu na kuchezesha viungo vyao wakati wakisoma na wakati huu wa mapumziko ya msimu wa joto ambapo michezo mingi imefungwa kwa sababu ya corona. “Yoga ni kitu tofauti kabisa , nimeona kilivyobadili maisha yangu na ya familia yangu. Yoga ina faida kubwa sana.” Amesema Nagaraj Naidu, naibu balozi wa kudumu wa India kwenye Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa uliitangaza Juni 21 kuwa siku ya kimataifa ya Yoga mwaka 2014 baada ya kupitishwa azimio namba 69/131 na Baraza Kuu la Umoja huo, na kuidhinisha maono yliyowasilishwa na waziri mkuu wa India Narendra Modi ambaye alikiambia kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba “Yoga inachagiza umoja wa mawazo na mwili kwa kuchukua mtazamo wa hatua ambao ni wa thamani kubwa kwa afya na ustawi.”