Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu lapitisha azimio kutaka ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wa asili ya Afrika ukomeshwe

Waandamanaji katika mitaa ya jiji la New York Marekani wakipinga ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa polisi kufuatia kifo cha George Floyd
UN Photo/Evan Schneider
Waandamanaji katika mitaa ya jiji la New York Marekani wakipinga ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa polisi kufuatia kifo cha George Floyd

Baraza la haki za binadamu lapitisha azimio kutaka ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wa asili ya Afrika ukomeshwe

Haki za binadamu

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet kuongoza juhudi za kushughulikia mfumo wa ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika unaofanywa na vyombo vya dola vya ulinzi na usalama.

Hilo limeamriwa leo Ijumaa na Baraza la Haki za Binadamu ambalo limepitisha kwa kauli moja azimio bila kura kufuatia mjadala wa dharura wa nadra kwenye Baraza hilo mapema wiki hii kwa ombi la kundi la mataifa ya Afrika kufuatia kifo cha George Floyd katika jimbo la Minnesota nchini Marekani.

Kifo cha Mmarekani mweusi huyo kilirekodiwa kwenye video wakati afisa wa polisi alipomkandamiza kwa goti lake kwa zaidi ya dakika nane mjini Minneapolisi na kusababisha maandamano makubwa kote duniani.

Mjadala wa azimio hilo

Wakati wa mjadala huo kuhusu ubaguzi wa rangi ukatili unaodaiwa kufanywa na polisi na ukatili mwingine dhidi ya waandamanaji ndivyo vilivyochochea kupitishwa kwa azimio hilo na wazungumzaji 120 walizungumza katika mjadala huo.

Wengi wa wawazungumzaji walitoa rambirambi zao kwa familia ya Bwana Floyd ambapo kaka yake pia alihutubia Baraza hilo na wajumbe mjini Geneva kwa njia ya video na ujumbe wake ulikuwa bayana aliutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua.

Ingawa baadhi ya wajumbe wametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuchunguza mauaji ya watu weusi nchini Marekani na ukatili dhidi ya waandamanaji , wengine wameshikilia kwamba suala hilo linaathiri mataifa yote na linahitaji mtazamo mpana zaidi.

Waandamanaji wakikusanyika katika eneo maarufu la Times Square jijini New York Marekani ili kudai haki na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani baada ya kifo cha George Floyd akiwa katika kizuizi cha polisi
Ann Sophie Persson
Waandamanaji wakikusanyika katika eneo maarufu la Times Square jijini New York Marekani ili kudai haki na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani baada ya kifo cha George Floyd akiwa katika kizuizi cha polisi

 

Azimio lililopitishwa

Kulingana na azimio hilo, Kamisha Mkuu wa Haki za binadamu anapaswa, “kuandaa ripoti ya mfumo maalum wa ubaguzi wa rangi, ukiukwaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu dhidi ya Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika unaofanywa na vyombo vya dola hususan yale matukio ambayo yamesababisha vifo vya George Floyd na Waafrika wengine au watu wenye asili ya Afrika”.

Azimio hilo pia limetaka Bi. Bachelet akisaidiwa na wataalam huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa na kamati “kutathimini hatua za serikali kwa watu waliokuwa wanaandamana kwa amani, wapitianjia na waandishi wa habari.”

Waliosimamia azimio hilo, Balozi Elisabeth Tichy-Fisslberger (Austria), Rais wa Baraza la Haki za binadamu  kwa mzunguko huu wa 14 walitangaza kwamba mswada wa azimio uko tayari kufikiriwa na kuuliza kama kura itakuwa ni ya lazima wakati kuna muafaka wa kauli moja.

“Waheshimiwa mabibi na mabwana  nimejulishwa kwamba maazimio kadhaa yako tayari kwa kupitishwa katika mkutano huu kama inavyoonesha kwenye kioo ..hivyo napenda kuwauliza endapo kuna ombi kutoka kwa yeyote la kura…sioni mkono wowote hivyo nichukulie kwamba mswada wa azimio namba L50 kama lilivyopitiwa kwa kauli huenda likapistishwa bila kura?...na hivyo ndivyo ilivyoamriwa.”

George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuaw baada ya kukamatwa na polisi nchini Marekani
UN News/Daniel Dickinson
George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuaw baada ya kukamatwa na polisi nchini Marekani

 

Kundi la Afrika

Katika hotuba yake kwa nchi wanachama mratibu wa kundi la Afrika Dieudonné W. Désiré Sougouri, mwakilishi wa kudumu wa Burkina Faso kwenye Umoja wa Mataifa amesema mjadala huo ni “hatua ya kihistoria katika kupambana na ubaguzi wa rangi ambayo Baraza la haki za binadamu linapaswa kujivunia.”

Ameongeza kuwa “ghadhabu ya kimataifa iliyochochewa na matukio ya kikatili na kusababisha kifo cha George Floyd inadhihirisha haja na umuhimu wa Baraza la Haki za binadamu kupaza sauti yake dhidi ya ukiukwaji wa haki na ukatili wa polisi dhidi ya Waafrika na watu wenye asili ya Afrika wanaokumbana nao kila siku katika maeneo mbalimbali duniani”

Baraza hilo pia limesikia uungwaji mkono mkubwa wa kutaka uchunguzi wa vitendo vya kikatili dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono maandamano ya vuguvugu la “Maisha ya watu weusi ni muhimu”.

 TAGS:HRC, Baraza la Haki za binadamu, ubaguzi wa rangi,